7 Januari 2021 - 10:01
Muuguzi aaga dunia siku 2 baada ya kupewa chanjo ya Covid-19 Ureno

Maafisa wa afya nchini Ureno wanachunguza kisa cha kufariki dunia ghafla muuguzi mmoja, saa 48 baada ya kupigwa chanjo ya kumkinga dhidi ya virusi vya corona.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Sonia Azevedo, mama wa watoto wawili aliyekuwa na umri wa miaka 41, alikuwa kati ya maafisa wa afya wapatao 538 waliokuwa miongoni mwa watu wa kwanza nchini humo kupokea chanjo ya shirika la Pfizer mjini Porto.

Muuguzi huyo aliyekuwa akifanya kazi katika Hospitali ya Watoto ya Upasuaji ya IPO mjini Porto, alipatikana ameaga dunia nyumbani kwake siku mbili baada ya kupigwa chanjo ya Covid-19.

Watu wa familia yake wanasema Azevedo hakuonekana na matatizo yoyote ya kiafya kabla ya kufariki kwake dunia. Babake mzazi aliyetambulika kwa jina la Abilioni ameliambia jarida la Orreio da Manha kuwa, "Nataka kujua nini kilichosababisha kifo cha binti yangu?  Alikuwa mzima wa afya na mwenye furaha usiku wa kuamkia siku alipokutikana ameaga dunia."

Binti ya muuguzi huyo, Vania Figueiredo ameliambia jarida hilo kuwa: Sikuona tofauti yoyote kwa mama yangu kabla ya yeye kuaga dunia. Alikuwa yu bukheri wa afya ingawaje alikuwa akisema kuwa anahisi maumivu katika mkono uliopigwa chanjo hiyo ya corona.

Haya yanajiri siku chache baada ya muuguzi mwingine katika jimbo la California nchini Marekani kuambukizwa virusi vya corona, zaidi ya wiki moja baada ya kupigwa chanjo ya kumkinga na maradhi ya Covid-19 ya kampuni hiyo ya Pfizer.

342/