25 Mei 2025 - 23:09
Source: Parstoday
Hamas: Shambulio la Israel lililoua watoto tisa wa daktari Gaza ni “ukatili wa kuogofya”

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imelaani shambulio la anga la jeshi katili la Israel lililolenga nyumba ya daktari wa Kipalestina, Alaa Al-Najjar, na kusababisha vifo vya watoto wake tisa kati ya kumi, ikilitaja tukio hilo kuwa “mauaji ya kutisha na ya kinyama.”

Katika taarifa yake siku ya Jumamosi, Hamas imesema kuwa shambulio hilo lililotokea Ijumaa liliikumba nyumba ya familia ya Dkt. Alaa katika mji wa Khan Yunis, kusini mwa Gaza, wakati alipokuwa kazini akihudumu katika hospitali.

Hamas imesema: “Uhalifu huu wa kinyama unaonesha wazi asili ya kikatili ya uvamizi huu, na kiwango cha chuki ya kisasi iliyozama ndani ya nafsi ya Netanyahu na genge lake la watekelezaji mauaji ya kinyama."

Hamas imeongeza kuwa tangu kuanza kwa vita dhidi ya Ukanda wa Gaza, Israel imekuwa ikilenga kwa makusudi wahudumu wa afya, raia na familia zao, kwa lengo la kuvunja moyo wa Muqawama na ustahimilivu wa watu wa Gaza.

Dkt. Alaa, ambaye ni daktari bingwa wa watoto katika Hospitali ya Nasser huko Gaza, alikuwa kazini akiwahudumia waathiriwa wa mashambulizi ya Israel wakati alipofahamishwa kuwa watoto wake tisa , wenye umri wa kati ya miaka miwili hadi 16 , wameuawa katika shambulio la anga lililolipiga nyumba yao eneo la Qizan al-Najjar, Khan Yunis.

Timu za uokoaji baadaye zilifukua miili ya watoto hao, ambapo miili ya wanane kati yao ilikuwa imeharibika vibaya kiasi cha kutotambulika kutokana na mlipuko huo.

Hamas: Shambulio la Israel lililoua watoto tisa wa daktari Gaza ni “ukatili wa kuogofya”

Kabla ya shambulio hilo, Dkt. Alaa alikuwa ameondoka nyumbani pamoja na mumewe, Hamdi al-Najjar, kuelekea kazini. Baada ya muda, Hamdi alirejea nyumbani peke yake, na ndipo shambulio hilo lilipotokea.

Nyumba yao iliharibiwa kabisa na moto ulienea katika maeneo ya jirani. Mume wa Dkt. Alaa pamoja na mtoto wao aliyenusurika walijeruhiwa katika tukio hilo.

Vikosi vya Israel vimekuwa vikilenga kwa mpangilio familia za raia, vituo vya afya, na wahudumu wa afya kama sehemu ya mauaji ya halaiki yanayoendelea Gaza.

Kwa mujibu wa Dkt. Muneer Alboursh, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya Palestina huko Gaza, Israel imewaua wahudumu wa afya 12 ndani ya wiki moja iliyopita pekee, wengi wao wakilengwa majumbani kwao kwa makusudi.

Israel ilianzisha mashambulizi hayo ya mauaji ya halaiki mnamo Oktoba 7, 2023. Tangu wakati huo, watu wasiopungua 53,900 wameuawa Gaza, kwa mujibu wa takwimu za wizara ya afya ya Gaza. Aghalabu ya waliouawa katika mauaji hayo ya kimbari yanayotekelezwa na Israel ni wanawake na watoto.

Aidha, vikosi vya Israel vinaendelea kutekeleza mzingiro kamili wa Gaza, vimefunga mipaka yote na kupunguza kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa misaada ya kibinadamu, mafuta na chakula.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha