Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO na Kituo cha Satelaiti cha Umoja wa Mataifa UNOSAT. Katika taarifa ya tathimini ya utafiti, taasisi hizo mbili zimesema: “Miundombinu ya kilimo katika Ukanda wa Gaza inaendelea kusambaratika kwa kasi ya kutisha, huku chini ya asilimia tano ya ardhi ya kilimo ikiwa ndiyo imesalia kwa matumizi yanayofaa.”
Kufikia Aprili 2025, mashirika hayo yamesema zaidi ya asilimia 80 ya ardhi yote ya kilimo Gaza ilikuwa imekwishaharibiwa, na karibu asilimia 78 ikiwa haiwezi kufikiwa na wakulima. Hali ni mbaya zaidi katika maeneo ya Rafah na kaskazini mwa Gaza, ambapo ardhi ya kilimo haifikiki kabisa kutokana na vita vinavyoendelea na vikwazo vya usafiri.
Ripoti hiyo pia inaonesha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya mifumo ya kilimo, ambapo zaidi ya asilimia 71 ya mifumo hiyo imeharibiwa.
FAO imesema Rafah imeathirika zaidi kwa kuongezeka uharibifu kutoka asilimia 57.5 mwezi Desemba 2024 hadi asilimia 86.5 kufikia Aprili 2025. Katika eneo la Gaza, hakuna kituo chcochote cha kilimo kilichosalia salama.
Aidha, karibu asilimia 83 ya visima vya umwagiliaji wa kilimo vimeharibiwa, kutoka asilimia 67.7 Desemba mwaka jana. Hasara hizi FAO inasema zimelemaza kabisa uwezo wa uzalishaji wa chakula wa ndani, uliokuwa ukitegemewa na jamii nyingi kuendesha maisha yao.
Mashirika hayo yamesema uharibifu huu unatokea wakati ambapo hofu ya baa la njaa inazidi kuongezeka. Tathmini ya karibuni ya viwango vya uhakika wa chakula IPC, inaonesha kuwa wakazi wote wa Gaza takribani watu milioni 2.1 wapo katika hatari kubwa ya kukumbwa na njaa.
Kati ya tarehe 1 Aprili hadi 10 Mei 2025, FAO imesema asilimia 93 ya wakazi walikuwa kwenye viwango vya janga au zaidi ya viwango vya IPC. Daraja la 3 au juu zaidi, wakiwemo watu 925,000 walioko katika "Hali ya Dharura ya viwango vya Daraja la 4, na watu 244,000 sawa na asilimia 12 wakiwa katika Daraja la 5 la janga la njaa, ambapo watu hukabiliwa na hali ya kutisha ya ukosefu wa chakula na hatari ya kufa kwa njaa.
Your Comment