3 Septemba 2025 - 23:42
Source: Parstoday
Pezeshkian ataka Iran na China zishirikiane katika kupinga ubabe wa kimataifa

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran, amesisitiza umuhimu wa kushirikiana na China katika kupinga vitisho na ushawishi wa upande mmoja kutoka kwa mataifa yanayojaribu kuvuruga uhusiano wa kirafiki kati ya nchi hizi mbili.

Akihitimisha ziara yake nchini China Jumatano, Pezeshkian amerejea Tehran baada ya kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai (SCO).

Rais Pezeshkian amesema: “Tunahitaji kupinga unyanyasaji wa mataifa yanayopinga uhusiano wa kirafiki kati ya Iran na China.” Pezeshkian ameyasema hayo alipokutana na Huang Hu, mshirika wa kudumu wa Chama cha Kikomunisti cha China.

Amesisitiza kuwa SCO ni jukwaa muhimu la kupinga ushawishi wa upande mmoja, na kwamba mataifa yanapaswa kuzingatia haki, usawa na kuheshimu sheria.

Rais Pezeshkian amesema kuwa ustaarabu wa dunia umetokana na historia tajiri na tamaduni za mataifa kama Iran na China, na kupitia urithi huo, mataifa yanaweza kuishi kwa heshima.

Ameongeza kuwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, ametoa maagizo ya kuipa China kipaumbele katika sera za kigeni za Iran, na kwamba kikundi cha kazi cha pamoja kitasimamia utekelezaji wa makubaliano ya pande mbili.

Rais wa China ametoa shukrani kwa tathmini chanya ya Iran kuhusu mkutano wa SCO mjini Tianjin, akisema Beijing iko tayari kutekeleza makubaliano hayo. Amesisitiza kuwa China itaendelea kuunga mkono Iran katika masuala ya uhuru wa kitaifa na maslahi ya kimkakati.

Viongozi wa China na Iran wamekubaliana kuongeza ushirikiano wa vitendo na kulaani mbinu za kulazimisha katika uhusiano wa kimataifa, wakisisitiza kuwa mataifa yao yanapinga utawala wa kimabavu na sera za kiimla.

Rais Pezeshkian mbali na kushiriki kikao cha SCO, pia amehudhuria gwaride ya kijeshi mjini Beijing ya kuadhimisha miaka 80 tangu kumalizika Vita vya Pili vya Dunia.

Mbali na mikutano hiyo, amefanya mazungumzo ya ana kwa ana na viongozi wa China, Russia, Uturuki, Tajikistan, Pakistan na pia kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres.

Your Comment

You are replying to: .
captcha