5 Novemba 2025 - 14:40
Source: Parstoday
Padri Mfaransa atuhumiwa kuwadhalilisha kingono wakimbizi watoto

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki la Rabat nchini Morocco jana aliliambia shirika la habari la AFP kuwa "ameshirikiana kikamilifu" na mamlaka za Morocco na nje ya nchi baada ya kasisi wa Ufaransa kutuhumiwa kwa kuwadhalilisha kingono wakimbizi watoto huko Casablanca.

Askofu Mkuu Cristobal Lopez Romero amebainisha haya siku mbili baada ya tovuti ya habari ya Morocco Enass kuripoti kuwa Padri Antoine Exelmans aliendesha "mfumo wa udhaliishaji wa kingono" uliowalenga watoto wahamiaji na wakimbizi katika kipindi cha kischopungua miaka minne.

"Mara tu taarifa za ukweli zilipofikishwa kwetu, tulichukua taratibu zinazohitajika kwa mujibu wa sheria za kanisa na tukashirikiana kikamilifu na mamlaka husika nchini Morocco na nje ya nchi", amesema Romero. 

Tovuti ya Enass imearifu kuwa, padri Exelmans mwaka 2016 alitumwa kufanya kazi katika Dayosisi ya Rabat nchini Morocco. 

Kulingana na tovuti hiyo, kesi hiyo inadaiwa kuwahusisha waathiriwa wasiopungua sita, wengi wao kutoka Guinea wakiwa na raia mmoja wa Cameroon. Romero alisema kanisa linafahamu kisa cha mwathiriwa mmoja.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, mwezi Septemba mwaka huu kundi la wahanga wa Padri mwingine wa Kifaransa kwa jina la Yves Grosjean ambaye alifungwa jela nchini Ufaransa kwa unyanyasaji wa kingono wa kupindukia lilikosoa ukimya" wa Dayosisi ya Dijon na Rabat, nakuwatuhumu maafisa wa kanisa kwa kutokuwa wawazi katika kushughulikia uhalifu huo wa kingono ulioripotiwa. 

Your Comment

You are replying to: .
captcha