Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la AhlulBayt (a.s) -ABNA- Uchunguzi mpya uliotolewa kutoka vyanzo fulani nchini Uingereza umefunua ukweli wa kushtusha kuhusu jinai zilizotekelezwa; jinai ambazo kinyume na madai ya “kupambana na ugaidi”, hazikuleta usalama Afghanistan, bali zinaonyesha kwamba baadhi ya wanajeshi wa kigeni waliendesha mambo kwa namna inayofanana na mifumo ya kimabavu. Neno “mifumo ya kimabavu” ndilo uchunguzi huu umetumia kusisitiza ukubwa wa uhalifu huu.
Kupigwa Risasi Watoto Wakiwa Wamelala - Uhalifu Uliofichwa kwa Muda Mrefu
Kwa mujibu wa taarifa ya Al-Ahed, uchunguzi huu unaonyesha kuwa vikosi maalum vya Uingereza katika matukio kadhaa viliwapiga risasi na kuwaua watoto wadogo Waafghani wakiwa kitandani.
Afisa mwandamizi wa vikosi maalum-anayetambulika kwa jina la siri N1466 - amesema katika ushahidi wake: “Huu ni uhalifu wa kivita. Hatupaswi kushuka mpaka kiwango cha mifumo ya kimabavu.”
Amefichua pia kuwa matukio mengi yalifichwa au kudhoofishwa uzito wake na makamanda wa vikosi maalum, na tahadhari zake kuhusu “saratan ya tabia isiyo ya kisheria” ndani ya kikosi fulani zilipuuzwa.

Mauaji ya Nje ya Sheria - Huenda Hii Ni Sehemu Ndogo Tu
Maafisa wengine pia wamethibitisha mbele ya kamisheni ya uchunguzi kwamba vikosi maalum nchini Afghanistan vilitekeleza mauaji ya nje ya mfumo wa sheria (EJK).
Afisa mmoja kwa jina la siri N5461 alisema: “Mauaji ya nje ya sheria yametokea. Na huenda haya ni ncha tu ya mlima wa barafu.”
Ushahidi huo unalingana na ripoti zilizowahi kutolewa kuwa baadhi ya waliokamatwa waliuawa baada ya kukamatwa kwa visingizio dhaifu, kama vile madai kwamba “walijaribu kushambulia baada ya kukamatwa.”
Visingizio Visivyoingia Akilini kwa Mauaji ya Waafghani
Afisa mwingine alidai kuwa baadhi ya waliokamatwa walikuwa “watumiaji sugu wa dawa za kulevya au walitaka kufa,” kama njia ya kuhalalisha idadi kubwa ya waliouawa—madai ambayo hata ndani ya jeshi la Uingereza yameonekana kutiliwa shaka.
Mfumo wa Kuficha Ukweli: Kuanzia Makamanda hadi Wizara ya Ulinzi
Nyaraka zinaonyesha kuwa baadhi ya makamanda na hata afisa mmoja wa juu serikalini hawakupatiwa taarifa muhimu kuhusu jinai hizi.
Ukimya huu ulioratibiwa unaibua maswali mazito kuhusu kiwango cha kuficha ukweli ndani ya jeshi la Uingereza.
Afghanistan: Mwathirika wa Mzunguko wa Ukatili Usio na Majibu
Ushahidi huu unaonyesha tena kwamba watu wa Afghanistan hawakuwa tu wahanga wa vita vya ndani au makundi yenye silaha ndani ya nchi, bali hata wanajeshi wa kigeni walikuwa sehemu ya mzunguko wa ukatili na kutokuwepo haki.
Ingawa serikali ya Uingereza inadai kuunga mkono “uchunguzi huru,” ushahidi umebainisha kuwepo kwa ukosefu mkubwa wa kuaminiana kati ya wanajeshi waliovujisha siri na makamanda wao.
Kwa nyakati zilizopita pia, uchunguzi na ripoti kama hizi zimewahi kuchapishwa katika vyombo vya habari vya Uingereza.

Your Comment