16 Juni 2026 - 01:00
John bin Huway (r.a): Mtumwa Mweusi Aliyeandika Historia ya Uaminifu kwa Imam Hussein (a.s)

Miongoni mwa mashujaa waliotukuka katika tukio la Karbala yupo John bin Huway (r.a.), ambaye historia yake inaonyesha wazi kwamba mbele ya Mwenyezi Mungu heshima ya mtu haipimwi kwa rangi, kabila wala hadhi ya kijamii, bali kwa imani, uchamungu na uaminifu kwa haki.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- John bin Huway (r.a) alikuwa shujaa wa Karbala mwenye asili ya Nubia ambaye, licha ya kuwa mtumwa wa zamani na mzee, alisimama kwa uaminifu usioyumba pamoja na Imam Hussein (a.s.) hadi akapata Shahada siku ya Ashura. Kisa chake kinaonyesha kwamba mbele ya Mwenyezi Mungu heshima ya mwanadamu haipimwi kwa rangi, kabila au hadhi ya kijamii, bali kwa imani, uchamungu, uaminifu na utayari wa kujitolea katika kutetea haki. 

Asili na Maisha ya Awali
John - kama ilivyodokezwa hapo juu - alikuwa mtu wa asili ya Nubia (Sudani ya kale) na awali alikuwa Mkristo. Baadaye alinunuliwa na sahaba mtukufu Abu Dharr al-Ghifari (r.a.), ambaye alimlea katika mazingira ya uadilifu na mapenzi kwa Ahlul-Bayt (a.s).

Baada ya Abu Dharr (r.a) kuhamishwa uhamishoni kwa amri ya Khalifa Uthman, John alielekea kwa Imam Ali bin Abi Talib (a.s.), ambaye alimpa uhuru wake (alimvua utumwa na kumuacha huru) na kumkaribisha miongoni mwa watu wake wa karibu (Masahaba wake).

Safari yake na Ahlul-Bayt (a.s.)
Baada ya kuuawa Shahidi kwa Imam Ali (a.s.), John aliendelea kuwa karibu na Imam Hasan al-Mujtaba (a.s.). Baada ya kifo cha Imam Hasan, alijiunga na Imam Hussein (a.s.) na akawa naye karibu katika safari kutoka Madina kwenda Makka, kisha kuelekea Iraq hadi Karbala.

Uaminifu Usioyumba
Imam Hussein (a.s.) alimweleza John kuhusu ugumu wa safari hiyo na hatima yake ya shahada. Hata hivyo, John hakusita wala kurudi nyuma.
Aliamua kubaki pamoja na Imam wake hadi mwisho, akiamini kuwa heshima ya kweli ni kufa katika njia ya haki.

Siku ya Ashura na Kauli ya Ujasiri
Siku ya A'shura, Imam Hussein (a.s.) alimpa John ruhusa ya kuondoka kutokana na umri wake na hali ya vita. Lakini John alikataa na akasema:
"Wallahi! Sitawaacha mpaka damu yangu hii nyeusi ichanganyike na damu zenu."

Kauli hii ilidhihirisha mapenzi yake makubwa kwa Ahlul-Bayt (a.s.) na utayari wake wa kujitolea kwa ajili ya haki.

Ushujaa Wake Uwanjani
Baada ya kupata ruhusa ya Imam Hussein (a.s.), John aliingia vitani huku akisoma mashairi ya hamasa yaliyosisitiza ulinzi wa kizazi cha Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Katika mapambano hayo, alionyesha ujasiri mkubwa na inasemekana aliwaua wapiganaji wapatao ishirini na watano kabla ya kuzingirwa na kuuawa Shahidi.

Dua ya Imam Hussein (a.s)
Baada ya kuuawa kwake, Imam Husayn (a.s.) alifika karibu na mwili wake na kumwombea dua ya heshima:
“Ewe Mwenyezi Mungu! Uufanye uso wake uwe mweupe, uufanye harufu yake iwe nzuri, mfufue pamoja na Mtume Muhammad (s.a.w.w.), na umjumuisha pamoja na Ahlul-Bayt wa Mtume.”
Riwaya zinaeleza kuwa dua hiyo ilikubaliwa na mwili wake ulipata harufu nzuri.

Somo Kutoka kwa Maisha yake
Kisa cha John bin Huway (r.a.) kinafundisha kuwa ubora wa mwanadamu haupimwi kwa rangi, kabila au hali ya kijamii, bali kwa:
1_Imani thabiti
2_Uaminifu kwa Mwenyezi Mungu
3_Kusimama upande wa haki
4_Kujitolea kwa ajili ya dini.

Nafasi yake katika Historia
John alikuwa mtumwa wa zamani, lakini alifika daraja la kuwa miongoni mwa mashahidi wa Karbala waliotukuka. Jina lake limehifadhiwa katika historia ya Ahlul-Bayt (a.s.) na hutajwa katika baadhi ya ziara kama Ziyarat an-Nahiyah al-Muqaddasah.

Hitimisho
John bin Huway (r.a.) ni mfano hai wa uadilifu, uaminifu na mapenzi yasiyoyumba kwa Ahlul-Bayt (a.s.). Maisha yake yanaendelea kuwahamasisha watu kusimama imara upande wa haki bila kujali rangi, asili au hali ya kijamii.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha