Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ismail Baqaei, amesema kuwa adui aliianzishia Iran hujuma kwa dhana kwamba angeweza kupata ushindi wa haraka, lakini mwishowe alikumbana na kushindwa na kuvunjika moyo.
Baqaei alisema kuwa maadui walitumia kuvunja ahadi zao kama njia ya kuzindua shambulio la kushtukiza dhidi ya Iran, wakilenga taifa ambalo kwa mujibu wa historia limejulikana kwa uimara wake, azma isiyoyumba na uwezo wa kuwashinda maadui wake.
Aidha, alieleza kuwa siku hiyo inaadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kuanza kwa mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni kwa uungaji mkono na ushiriki wa Marekani. Alisema mashambulizi hayo yaliambatana na mauaji aliyoyataja kuwa ya kinyama yaliyowalenga watetezi wa taifa pamoja na kushambuliwa kwa baadhi ya vituo vya nyuklia vya Iran.
Msemaji huyo alisisitiza kuwa uimara wa wananchi wa Iran, kujitolea kwao na azma yao thabiti vilifanikisha kuvuruga malengo ya washambuliaji na kugeuza matarajio yao ya ushindi kuwa kushindwa na kufeli.
Baqaei alihitimisha kwa kusema kuwa historia imeonyesha kuwa Iran imeendelea kusimama imara mbele ya mashinikizo na vitisho, na kwamba haitasalimu amri mbele ya hujuma dhidi ya mamlaka na uhuru wake.
Your Comment