Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) - ABNA - Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu, Jagan Chapagain, amepongeza utendaji wa kipekee wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa makabiliano ya hivi karibuni.
Chapagain ameeleza kuwa shughuli za uokoaji, utoaji wa huduma za matibabu, juhudi za utafutaji na uokoaji pamoja na kujitolea kwa wanachama na watu wanaojitolea, ni mfano muhimu unaoonyesha uwezo wa mashirika ya kitaifa yenye nguvu katika kukabiliana na majanga na migogoro.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran (IRNA), akimnukuu Hilali Nyekundu ya Iran, Chapagain alimtumia ujumbe Rais wa Jumuiya ya Kitaifa ya Hilali Nyekundu ya Iran, Pirhossein Kolivand, akieleza kuthamini kwake mwitikio wa kibinadamu uliotolewa na Hilali Nyekundu ya Iran katika mazingira ya migogoro inayoendelea.
Afisa huyo wa kimataifa ameeleza kuwa Hilali Nyekundu ya Iran imekabiliana na changamoto kubwa za kiutendaji, vifaa na kibinadamu, akisema kuwa taasisi hiyo, ikiwa mhusika mkuu wa shughuli za kibinadamu nchini Iran, imeonyesha uongozi thabiti na wenye ufanisi.
Amesema uratibu wa huduma za dharura za afya, utekelezaji wa shughuli za uokoaji saa 24 kwa siku, utoaji wa msaada wa kisaikolojia na kijamii pamoja na mawasiliano madhubuti na jamii za maeneo yaliyoathirika, ni miongoni mwa juhudi zilizotekelezwa na Hilali Nyekundu ya Iran.
Aidha, amesifu shughuli za utafutaji na uokoaji zilizofanywa kwa ujasiri na weledi mkubwa, akisema kuwa juhudi hizo haziakisi tu uwezo wa kitaalamu, bali pia zinaonyesha kiwango kikubwa cha imani ambacho wananchi wanayo kwa Hilali Nyekundu ya Iran.
Chapagain amesisitiza kuwa utendaji wa Hilali Nyekundu ya Iran ni mfano bora wa uwezo wa mashirika ya kitaifa yenye nguvu katika kukabiliana na majanga.
Ameongeza kuwa juhudi hizo zimesaidia kuokoa maisha ya watu, kupunguza mateso na kulinda utu wa kibinadamu wakati wa hali ngumu.
Katibu Mkuu huyo wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu amesema shirikisho hilo litaendelea kusimama pamoja na Hilali Nyekundu ya Iran, wafanyakazi wake na mtandao wake mpana wa watu wanaojitolea.
Amesema ujasiri na kujitolea kwa wafanyakazi na wanachama wa Hilali Nyekundu ya Iran vinaendelea kuwa chanzo cha hamasa kwa wanachama wote wa mtandao wa kimataifa wa Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu.

Maoni yako