Maelfu ya Wapalestina walikusanyika leo kuomboleza kifo cha waziri wao aliyeuawa wakati wa makabiliano ya waandamanaji na wanajeshi wa Israel, wakati wanajeshi zaidi wakipelekwa katika Ukingo wa Magharibi na kujiandaa kwa vurugu.
Uongozi wa Palestina umeilaumu Israel kwa kifo cha Ziad Abi Ein aliyekuwa na umri wa miaka 55, wakati mvutano ukitishia kuzusha duru mpya ya machafuko katika maeneo hayo. Abu Ein waziri asiye na wizara maalum, alifariki dunia hapo jana baada ya kukabiliana na wanajeshi wa Israel wakati wa maandamano ya karibu Wapalestina 300 kupinga ujenzi wa makaazi ya Wayahudi. Waandamanaji hao walitaka kupanda miti ya mizeituni katika eneo hilo. Wataalamu wa Palestina na Israel hawakukubaliana juu ya sababu za kifo cha waziri huyo. Maafisa wa Palestina wanailaumu Israel wakisema uchunguzi umeonyesha alifariki dunia kutokana na gesi ya kutoa machozi na kupigwa na wanajeshi wa Israel.
Kuawa kwa waziri huyu kunaashiria uwezekano wa kutokea machafuko makubwa zaidi baina ya waparestina na waisrael.