Serikali ya Marekani imesema kwamba wafungwa 64 kati ya 132 wanaobakia katika gereza ka Guantanamo Bay wanaweza kuondoka katika gereza hilo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya nchi hiyo Marie Harf amesema Marekani inasubiri nchi nyingine zikubali kuwapokea wafungwa hao.
Mapema mwezi huu, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, John Kerry, aliyaomba makao makuu ya Kanisa Katoliki mjini Vatican kusaidia kupatikana kwa suluhisho la kibinadamu kuhusu wafungwa hao wa Guantanamo.
Mjumbe maalum wa Marekani kuhusu kufungwa kwa gereza hilo, Cliff Sloan, ambaye ametangaza kujiuzulu wadhifa wake, alifanikiwa kupata mahali pa kuwapeleka wafungwa 34 mnamo miezi 18 alipokuwa katika wadhifa huo. Alipoingia madarakani mwaka 2009, Rais Barack Obama aliahidi kulifunga gereza la Guantanamo, lakini hakuweza kuitekeleza ahadi hiyo kwa kukosa mahali pa kuwapeleka wafungwa wanaoshikiliwa huko.
Marekani imelaumiwa sana na mataifa kutokana na adhabu za kinyama ilizokuwa ikiwadhibu wafungwa waliyoko katika gereza hilo lenye kutisha, na mpaka sasa inasubiriwa ripoti maalum inayo onyesha jinsi serikali ya Marekani ilivyokeuka haki za binadamu kwa wafungwa hao. Marekani inahofu kama ripoti hiyo itaelezea hali halisi ya adhabu na mateso kama ilivyokuwa katika gereza hilo la Guantanamo huenda ikasababisha chuki na uadui usioisha dhidi ya serikali ya Marekani.