Chama tawala nchini Burundi kimemwidhinisha leo Rais Pierre Nkurunziza kugombea muhula wa tatu madarakani, licha ya kuongezeka maandamano ya kupinga hatua hiyo ambayo upinzani unasema ni kinyume cha sheria.
Mkuu wa chama tawala cha CNDD FDD Pascal Nyabenda alisema katika mkutano mkuu wa Chama hicho kuwa mgombea aliyeteuliwa kukiwakilisha chama ni Nkurunziza ambaye ana haki ya kuchaguliwa tena. Kulikuwa na hofu kuwa mgogoro huo wa kisiasa, ambapo chama tawala cha Nkurunziza CNDD FDD kimeshutumiwa kwa kuwakandamiza wapinzani, huenda ukairudisha Burundi katika machafuko.
Taifa hilo limeupatia ufumbuzi mzozo wake wa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka wa 2006. Upinzani umeapa kuendelea kuandamana ili kupinga hatua ya Nkurunziza kushiriki katika uchaguzi wa rais wa Juni 26. Unahoji kuwa hatua ya Nkurunziza kutaka kugombea tena inakiuka katiba pamoja na makataba wa amani uliosainiwa mjini Arusha, ambao ulimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.