15 Julai 2025 - 23:44
Hapana kwa Hotuba za Chuki: Hadithi ya Unyanyasaji wa Kibaguzi nchini Uhispania Dhidi ya Wahamiaji wa Morocco

Shambulio dhidi ya mzee mmoja katika mji wa Torrepacheco katika eneo la Murcia nchini Uhispania limezusha wimbi la ghasia za kibaguzi, huku makundi ya mrengo wa kulia yakitumia tukio hilo kuchochea chuki dhidi ya wahamiaji wa Morocco. Ripoti hii inachunguza chimbuko la tukio, matokeo yake na juhudi zinazoendelea za kudhibiti mgogoro huo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Mnamo tarehe 9 Julai 2025, Domingo, mwanaume mwenye umri wa miaka 68, alishambuliwa kwa ukatili na kundi la vijana wakati wa matembezi yake ya asubuhi karibu na makaburi katika mji mdogo wa Torre-Pacheco, eneo la Murcia, Uhispania. Shambulio hilo halikufanywa kwa nia ya uporaji bali lilionekana kuwa ni shambulio kwa ajili ya kurekodi videona kuirusha katika mitandao ya kijamii.

Video fupi ya sekunde 25 ilisambaa kwenye mtandao wa X ikidai kuonyesha tukio hilo, lakini baadaye ilithibitishwa kuwa ni tukio tofauti lililotokea mwezi Mei 2025 huko Almería (Almería ni mji na manispaa ya Uhispania, iliyoko Andalusia) kwa mhanga mwingine aliyeitwa José. Kutokana na mkanganyiko huo, habari za uongo zilisambaa kwa kasi.

Matamshi ya Domingo kwamba washambuliaji walizungumza lugha ya kigeni (labda kutoka Morocco) yalikumbatiwa na makundi ya mrengo wa kulia, hasa chama cha Vox, kama kisingizio cha kuchochea chuki dhidi ya wahamiaji, hasa Wamoroko. Vikundi kama Deport Them Now vilisambaza picha na taarifa za uongo, na kupanga "mikusanyiko ya kuwawinda wahamiaji" tarehe 15 hadi 17 Julai.

Maandamano yaliyofanyika tarehe 11 Julai kwa kaulimbiu "Torre-Pacheco bila Ukatili na Uhalifu" yaligeuka vurugu baada ya watu kutoka nje ya mji, wakiwemo wa mrengo mkali wa kulia, kuingilia. Kauli za chuki, mashambulizi ya mawe na chupa, pamoja na vurugu za mitaani zilifuata, haswa katika eneo la San Antonio ambako wakaazi wengi ni wahamiaji.

Katika siku zilizofuata, mashambulizi dhidi ya maduka na magari ya wahamiaji yaliripotiwa. Vijana Wamoroko, hasa wa kizazi cha pili, waliingia katika makabiliano na washambuliaji, hali iliyosababisha watu watano kujeruhiwa na watu 10 kukamatwa, akiwemo mshukiwa mkuu aliyekamatwa akiwa njiani kukimbilia Ufaransa.

Mamlaka za usalama ziliingilia kwa haraka: askari wa vikosi maalum walitumwa, barabara kuu za kuingia mjini zikafungwa, na uchunguzi ukaanzishwa dhidi ya wachochezi wa ghasia na matamshi ya chuki. Waziri wa Mambo ya Ndani, Grande-Marlaska, alilaumu chama cha Vox kwa kuchochea chuki.

Meya wa mji huo, Pedro Ángel Roca, alitangaza hatua za usalama kama kuongeza ulinzi wa polisi na kufunga kamera za ulinzi. Nabil Moreno, kiongozi wa Waislamu wa Torre-Pacheco, alisisitiza umuhimu wa kuishi kwa amani pamoja, akieleza kuwa vijana wa kizazi cha pili wanakumbwa na hali ya kutengwa na dhuluma za kijamii.

Hali ya sasa: Hadi kufikia tarehe 15 Julai 2025, hali ya tahadhari bado imetanda Torre-Pacheco. Wakaazi, hasa wa eneo la San Antonio, wanaishi kwa hofu. Maduka yanafungwa mapema na polisi wameweka doria kila kona. Uchunguzi bado unaendelea dhidi ya wahusika wa shambulio na wachochezi wa ghasia za kibaguzi.

Tukio hili limedhihirisha jinsi tukio dogo linaweza kuchochewa kisiasa na kupitia mitandao ya kijamii kuwa mzozo mkubwa wa kijamii. Katika mji huu ambako wahamiaji ni thuluthi moja ya wakazi 40,000, juhudi za kurejesha amani na mshikamano zinaendelea huku kivuli cha chuki na ubaguzi kikiendelea kutanda.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha