Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Al-Mustafa (s.a.w) na Chuo Kikuu cha Félix Houphouët-Boigny cha Abidjan vimesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kielimu na kufanya maboresho ya makubaliano ya ushirikiano yaliyopo kati yao.
Katika kikao rasmi kilichofanyika Jumatano, tarehe (17 Desemba 2025), katika ofisi ya uongozi wa Chuo Kikuu cha Félix Houphouët-Boigny, Dkt. Ruhullah Ibrahimi, Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Al-Mustafa – Côte d’Ivoire, alikutana na Profesa Balo Zié, Rais wa Chuo Kikuu cha Félix Houphouët-Boigny. Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Bwana Sayyid Gholamreza Meigouni, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Côte d’Ivoire.
Katika mkutano huo, pande zote mbili zilikubaliana juu ya haja ya kuimarisha mahusiano ya kielimu, kupanua ushirikiano wa kitaaluma, na kusasisha makubaliano ya ushirikiano kati ya vyuo hivyo viwili ili yaendane na mahitaji ya sasa ya elimu ya juu.
Aidha, iliamuliwa kuwa Rais wa Chuo Kikuu cha Félix Houphouët-Boigny atafanya ziara rasmi ya karibu katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Al-Mustafa - Côte d’Ivoire, akiwa ameambatana na ujumbe rasmi, kwa lengo la kuimarisha zaidi misingi ya ushirikiano hai na wa pande zote.
Mkutano huu unaakisi nia ya dhati ya pamoja ya vyuo hivyo viwili katika kuinua ubora wa elimu ya juu, kupanua ushirikiano wa baina ya vyuo vikuu, na kubadilishana uzoefu wa kielimu nchini Côte d’Ivoire.

Your Comment