1 Juni 2019 - 08:45
Nasrallah: Vita dhidi ya Iran vitawasha moto eneo zima

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ametahadharisha kuwa vita dhidi ya Iran havitaishia katika mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu bali vitawasha moto katika eneo zima la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).

(ABNA24.com) Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ametahadharisha kuwa vita dhidi ya Iran havitaishia katika mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu bali vitawasha moto katika eneo zima la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).

Akizungumza Ijumaa usiku kwa njia ya Televieheni kutoka Beirut kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds, Sayyed Hassan Nasrallah amesema propaganda za vita dhidi ya Iran zimepungua baada ya Rais Donald Trump wa Marekani na maafisa wake wa kijasusi kubaini kuwa, vita vyovyote dhidi ya Iran vitawasha moto eneo zima. Aidha amesema maslahi yote ya Marekani yataangamizwa iwapo vita kama hivyo vitazuka kama ambavyo waliochochea vita hivyo, yaani utawala wa Israel na Saudia Arabia nao pia watapata hasara kubwa.

Kiongozi wa harakati ya Hizbullah hali kadhalika amesema iwapo vita vitazuka katika eneo, bei ya mafuta ghafi ya petroli duniani itaongezeka kufika dola 200 hadi 300 kwa pipa. Hivi sasa pipa moja la mafuta ni karibu dola 68.

Kiongozi wa Hizbullah amesema si kwa maslahi ya Trump kuona kuna uhusiano mzuri baina ya Iran na nchi za Ghuba ya Uajemi kwani maslahi yake yako katika kuwafanya watawala wa nchi za Ghuba waiogope Iran sambamba na kuendeleza vita vya kiuchumi baina ya Iran na mataifa mengine.  

Katika hotuba yake, Sayyid Hassan Nasrallah pia amelaani mpango wa  Trump wa Marekani wa kile anachodai kuwa 'amani Mashariki ya Kati'. Amesema kile ambacho Trump anakitaja kuwa ni  'Muamala wa Karne ni batili na jinai ya kihistoria.

Amesema muamala huo ukitekelezwa utakuwa ni hasara kwa haki za Kiislamu, Palestina na Waarabu. Ameongeza kuwa ni jukumu la kidini, kimaadili, kitaifa na kisiasa kupinga mpango huo wa Trump kwani ni wa kidhalimu na unakiuka haki za maeneo matakatifu.

Kiongozi wa Hizbullah pia amesema, leo ikiwa imepita miaka 40 tokea Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aitangaze Ijumaa ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds, siku hii inazidi kupata umashuhuri duniani pamoja na kuwepo njama za maadui za kutaka kuidhoofisha au kuisahaulisha.




/129