(ABNA24.com) Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amehutubia mkutano wa 18 wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungama na Siasa za Upande Wowote NAM mjini Baku, mji mkuu wa Azerbaijan na kueleza kwamba, njia ya kujinasua na migogoro ni kuheshimu uwajibikaji, kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kuandaa mazingira mwafaka kwa ajili ya mazungumzo na ushirikiano.
Rais Rouhani ameashiria nukta muhimu katika hotuba yake hiyo ikiwemo ishara yake ya siasa za kupenda vita za Marekani katika eneo hili la Asia Magharibi ambazo zimezisababishia nchi nyingine hasara ya mabilioni ya dola. Rais Rouhani amesema kuwa, upendaji huu wa vita umesababisha kuota mizizi fitna na ugaidi.
Kimsingi ni kuwa, siasa za upande mmoja za Marekani zimesababisha kuibuka vita na kushtadi mizozo na mivutano sambamba na kuongezeka vitendo vya utumiaji mabavu na kuibuliwa mifarakano katika mahusiano ya kieneo na kimataifa bila kusahau kubakia nyuma kiuchumi. Kwa mtazamo wa weledi wa mambo ni kuwa, Jumuiya ya Nchi Zisizofungama na Siasa za Upande Wowote NAM kwa kifupi ina uwezo wa kutosha wa kufanikisha lengo hili lakini kutokana na sababu mbalimbali imeshindwa kunufaika na fursa hiyo.
Abul-Qassim Qassimzadeh mweledi wa masuala ya kisiasa anaamini kuwa: Licha ya kuwa katika eneo la Asia Mashariki kuna mikataba ya kieneo yenye nguvu, lakini kwa upande wa eneo la Asia Magharibi kutokana na eneo hili kugubikwa na migogoro na vita, limeshindwa kupata mshikamano wa kieneo kupitia mikataba yake ya kieneo.
Hotuba ya Rais Hassan Rouhani katika mkutano wa NAM nayo iliashiria nukta hii kwamba, kutokea vita na kuweko uvamizi sambamba na kutokomezwa fursa za ukuaji na ustawi ni miongoni mwa matatizo ambayo nchi za eneo hili zimetwishwa na kubebeshwa.
Katika uwanja huu, nafasi ya nchi 120 wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote kwa ajili ya kukabiliana na mwenendo huu ni muhimu na ya kuzingatiwa mno. Jumuiya ya NAM tangu ilipoanzishwa mwaka 1961 licha ya mapungufu na udhaifu uliopo kwa baadhi ya nchi wanachama, lakini katika upande wa mtazamo wake juu ya masuala ya kimataifa imefanya juhudi kubwa na kuwa na nafasi muhimu kutokana na kuchukua misimamo ya maana na ya kimsingi kuhusiana na amani na usalama wa dunia.
Wanachama wa jumuiya hii mbali na upande wa kisiasa wamekuwa na nafasi muhimu na athirifu pia katika masuala ya kiuchumi ambapo kuweko mitazamo mimoja kunaweza kuibadilisha kambi hii na kuwa amilifu katika eneo. Hapana shaka kuwa, mitazamo hii ya pamoja ina taathira chanya pia katika uga wa kisiasa.
Akihutubia pia katika mkutano wa tano wa Ushirikiano na Uchukuaji Hatua za Kuleta Hali ya Kuaminian Asia (CICA) uliofanyika huko Tajikistan, Rais Hassan Rouhani sanjari na kubainisha misimamo ya Iran alisema kuwa: Katika mazingira ya sasa ya dunia, ili kufikia kiwango cha amani na ustawi unaokubalika, kuna haja ya kuweko ushirikiano na mazungumzo ya kieneo yenye lengo la kukuza maelewano.
Katika kalibu hiyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipendekeza katika Mkutano Mkuu wa 68 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) juu ya kuweko 'Ulimwengu wa Kukabiliana na Utumiaji Mabavu na Kufurutu Ada' ambapo hilo lilipelekea kupasishwa maazimio mawili ya kijamii katika Baraza Kuu la umoja huo katika miaka ya 2013 na 2015.
Katika mkutano wa mwaka huu pia wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Rais wa Iran aliwasilisha pendekezo la 'Hatua ya Amani ya Hormuz' kwa ajili ya usalama na uthabiti katika eneo, lengo lake likiwa ni kukuza kiwango cha usalama, uthabiti, maendeleo, kuanzisha maelewano ya pande kadhaa na mahusiano ya amani na urafiki wa nchi za Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz.
Tab'an, kufanikiwa malengo mengine ya Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM kama haki halali ya kujitetea, haki ya ustawi na maendeleo ya kielimu na kustafidi na harakati za kibiashara na kiuchumi, au haki ya kuwa na ardhi na kurejea katika ardhi za mababu zao wananchi madhulumu wa Palestina ni mambo yenye kuhitajia ushirikiano imara zaidi miongoni mwa nchi wanachama.
Hotuba ya Rais Hassan Rouhani katika mkutano wa 18 wa Jumuiya ya NAM uliofanyika Baku Azerbaijan kwa upande huu inabainisha mikakati na mapendekezo ya Iran kuhusiana na amani na usalama wa dunia.
/129
Hotuba ya Rais Rouhani katika mkutano wa NAM; sisitizo la udharura wa kuimarishwa amani na usalama wa eneo
26 Oktoba 2019 - 09:46
Msimbo wa Habari: 984505
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amehutubia mkutano wa 18 wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungama na Siasa za Upande Wowote NAM mjini Baku, mji mkuu wa Azerbaijan na kueleza kwamba, njia ya kujinasua na migogoro ni kuheshimu uwajibikaji, kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kuandaa mazingira mwafaka kwa ajili ya mazungumzo na ushirikiano.