(ABNA24.com) Awamu ya kwanza ya maandamano hayo ilianza tarehe Mosi Oktoba na kusimama wakati wa kukaribia kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein AS. Awamu ya pili ya maandamano hayo iliyoanza tarehe 25 Oktoba ingali inaendelea. Kilio na matakwa makuu ya wananchi wa Iraq ni kuboreshwa hali ya maisha na huduma za kijamii na kuweko mapambano na vita vya kweli va serikali dhidi ya ufisadi.
Pamoja na hayo, kuanza malalamiko ya wananchi wa Iraq kulikwenda sambamba na njama za baadhi ya madola ya kigeni za kutaka kuyabadilisha matakwa hayo ya kiuchumi na kijamii ya wananchi na kuwa ya kisiasa.
Marekani ni moja ya madola hayo ya kigeni ambayo ikitumia ushawishi ilionao kwa baadhi ya shakhsiya wa Kiiraqi, imefanya juhudi na njama kubwa za kubadilisha matakwa ya wananchi hayo na kuyasukuma upande wa kisiasa.
Katika fremu hiyo na katika taarifa yake ya karibuni kabisa, Ikulu ya Marekani White House imeitaka serikali ya Iraq isitishe hatua zake za kuwakandamiza waandamanaji na iitishe pia uchaguzi wa mapema.
Taarifa hiyo ya Ikulu ya Marekani White House inatolewa katika hali ambayo, kwa upande mmoja malalamiko ya wananchi wa Iraq yamechukua mkondo wa kupungua na katika upande wa pili, wananchi wa nchi hiyo na makundi mengine ya kisiasa yamefikia natija hii kwamba, yaipatie serikali ya Waziri Mkuu Adil Abdul-Mahdi al-Muntafiki fursa ili atekeleze vifurishi vya mapendekezo ya mageuzi. Kwa maneno mengine ni kuwa, suala la kufanyikka uchaguzi wa kabla ya wakati siyo chaguo linalozungumziwa kabisa kwa sasa na makundi ya nchi hiyo.
Takwa hilo la White House limekabiliwa na radiamali na upinzani mkali wa makundi ya Iraq. Ayatullah Sayyid Ali Sistani, Kiongozi wa Kidini na Marjaa Taklidi wa nchini Iraq alisema katika mazungumzo yake Jumatatu ya juzi na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Iraq kwamba, madola ya kigeni yanapaswa kuheshimu mamlaka ya kujitawala nchi hiyo na akasisitiza udharura wa madola ya kigeni kujiepusha na uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Sayyid Muqtada Sadr, Kiongozi wa Mrengo wa Sadr nchini Iraq naye juzi usiku alitoa taarifa rasmi akitangaza upinzani wake dhidi ya kufanyika uchaguzi wa kabla ya wakati kwa usimamizi wa Marekani na akatangaza waziwazi kwamba, Iraq haina haja na madola ya kibeberu na kama Washington itaingilia tena masuala ya ndani ya nchi ya Baghdad, basi kutafanyika maandamano ya mamilioni ya wananchi dhidi ya taifa hilo la kibeberu.
Qais Khazali, Katibu Mkuu wa Harakati ya Asa'ib Ahl al-Haq (AAH) amesema kuwa, taarifa ya White House inaonyesha kuwa, pendekezo la kufanyika uchaguzi wa kabla ya wakati, kimsingi ni mpango wa Marekani ambapo sasa kunafanyika juhudi za kuuhuisha. Inaonekana kuwa, lengo la Marekani la kuishinikiza serikali ya Iraq ili iitishe uchaguzi wa mapema ni kutaka kuendelea machafuko na ukosefuu wa uthabiti wa kisiasa na kiusalama katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Dhana ya Marekani ni hii kwamba, kuendelea mazingira ya sasa yanayotawala nchini Iraq, yataifanya serikali na Jeshi la Kujitolea la Wananchi la Hashd al-Sha'abi kujikita zaidi na masuala ya ndani na hivyo kutojihusisha sana na masuala ya kieneo hususan matukio ya Syria.
Baadhi ya shakhsiya kama Muqtada Sadr, Kiongozi wa Mrengo wa Sadr wanaamini kuwa, hatua ya Marekani ya kutaka kufanyika uchaguzi wa mapema ina lengo la kudandia mawimbi ya malalamiko ya wananchi wa Iraq na kuigeuza nchi hiyo iwe kama Syria. Kwa maneno mengine ni kuwa, Marekani inafanya njama za kuiingiza Iraq katika marhala na hatua ya machafuko ya ndani katika mhimili wa vurugu na mizozo baina ya Mashia.
.........
340