Main Title

source : Parstoday
Jumapili

4 Septemba 2022

18:25:53
1303333

Mali yawaachia askari watatu wa Ivory Coast, 46 wangali wako kizuizini

Mali imewaachia huru askari watatu wanawake kati ya askari 49 wa Ivory Cooast waliokamatwa na kuwekwa kizuizini nchini humo.

Askari hao wanawake walifika nyumbani jana usiku zikiwa zimepita takribani wiki saba tangu wao na wenzao wanaume 46 walipokamatwa, hatua ambayo imezusha mzozo wa kidiplomasia kati ya Mali inayotawaliwa na jeshi na Ivory Coast.Serikali ya kijeshi ya Mali ilisema, kundi la askari hao - ambao walizuiliwa katika uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Mali, Bamako mnamo Julai 10 - waliingia nchini humo bila kibali na walihesabiwa kuwa ni mamluki.Ivory Coast, ambayo imekuwa ikiomba mara kwa mara askari wake waachiliwe huru, inasema wanajeshi hao hawakustahiki kukamatwa kwa sababu walitumwa kwenda kutoa msaada kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Mali, MINUSMA. Serikali ya Yamoussoukro inasisitiza kuwa, mamlaka za Mali zina taarifa kamili kuhusu majukumu yaliyokuwa yatekelezwe na wanajeshi hao.Kanali Assimi Goita

Waziri wa Mambo ya Nje wa Togo Robert Dusse, ambaye nchi yake imekuwa ikiongoza mazungumzo ya usuluhishi baina ya Mali na Ivory Coast aliwaambia waandishi wa habari hapo jana kwamba wanawake hao watatu "waliachiliwa kama ishara ya ubinadamu" ambayo imeonyeshwa na kiongozi wa kijeshi wa Mali, Kanali Assimi Goita.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Togo ameongeza kuwa, majadiliano yanaendelea ili kuhakikisha askari wengine waliowekwa kizuizini wanaachiwa huru haraka.Dusse alikuwa akizungumza katika mji mkuu wa Togo, Lome, akiwa pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Mali, Abdoulaye Diop na mkurugenzi wa baraza la mawaziri la Ivory Coast, Fidele Sarassoro.Sarassoro ameeleza kuwa, Ivory Coast inaamini sutafahamu na kutoelewana ndio chanzo cha tukio hilo, ambalo amesema ni la kusikitisha sana.Kukamatwa wanajeshi wa Ivory Coast lilikuwa tukio la karibuni zaidi la mvutano kati ya kiongozi wa kijeshi wa Mali na jamii ya kimataifa. Goita amekabiliwa na hali ya kuzidi kutengwa baada ya kunyakua madaraka katika mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika miaka miwili iliyopita na kisha kushindwa kutekeleza muhula aliopewa kimataifa wa kuandaa uchaguzi mpya wa kidemokrasia nchini Mali.../


342/