Main Title

source : PARSTODAY
Alhamisi

13 Oktoba 2022

18:46:35
1313409

Ajali ya boti yaua watu 27 Kongo DR, 32 wametoweka

Kwa akali watu 27 wameaga dunia baada ya boti iliyokuwa imewabeba kuzama katika Mto Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hayo yalisemwa jana na msemaji wa mkoa wa  Equateur, Luc-Didier Mbula ambaye amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu akisema kuwa, boti hiyo ilipinduka usiku wa kuamkia jana katika eneo la Wendji-Secli, yapata kilomita 20 kusini magharibi mwa mji wa Mbandaka.

Amesema maiti 27 zikiwemo za watoto zimeopolewa kutoka majini, huku manusura 60 wakiokolewa. Mbula ameongeza kuwa, boti hiyo ilikuwa imebeba abiria wapatao 120.

Duru za habari zinaarifu kuwa, boti hiyo iliyokuwa imbeba abiria na mizigo ilipinduka kutokana na upepo mkali.

Akthari ya wananchi wa DRC hutumia usafiri wa boti kutokana na mfumo mbaya wa barabara za nchi hiyo ya katikati mwa Afrika. Ajali za boti huripotiwa mara kwa mara nchini humo.

Boti chakavu za mbao ndizo zinazotumika zaidi kusafirisha watu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mara nyingi boti hizo hujaza watu na mizigo kupita kiasi, husafiri nyakati za usiku na hazina kinga zozote za kutoa dhamana ya kufika salama zinakokwenda.

Hivi karibuni, watu wasiopungua 55 waliaga dunia baada ya boti iliyokuwa imewabeba kuzama katika Mto Congo, kaskazini mwa mkoa wa Mongala.

342/