Main Title

source : Parstoday
Jumapili

6 Novemba 2022

20:27:48
1320959

WHO: Afya iwe msingi wa majadiliano ya mabadiliko ya tabianchi COP27

Wakati mazungumzo muhimu ya mabadiliko ya tabianchi COP27, yanaanza leo huko Sharm-el Sheikh nchini Misri, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO, limekumbusha kwamba mzozo wa mabadiliko ya tabianchi unaendelea kuwafanya watu kuwa wagonjwa na kuhatarisha maisha na kwamba afya lazima iwe msingi wa mazungumzo hayo muhimu.

WHO inaamini kuwa mkutano huo lazima umalizike kwa mafanikio katika malengo muhimu kukiwemo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ufadhili na ushirikiano ili kuweza kupunguza athari za janga la mabadiliko ya tabianchi.

WHO imesema COP27 itakuwa fursa muhimu kwa ulimwengu kuja pamoja na kujitolea tena kuhuisha lengo la makubaliano ya Paris la kuhakikisha kiwango cha joto kinasalia kuwa nyuzi joto 1.5 °C.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhamon Ghebreyesus amesema "Mabadiliko ya tabianchi yanafanya mamilioni ya watu kuwa wagonjwa au kuwa katika hatari zaidi ya magonjwa duniani kote na uharibifu unaoongezeka wa matukio ya hali ya hewa huathiri vibaya jamii maskini na zilizotengwa. Ni muhimu kwa viongozi na watoa maamuzi wanaokutana katika COP27 kuweka afya katika kiini cha mazungumzo."

Ameongeza kuwa “Afya yetu inategemea afya ya mifumo ya ikolojia inayotuzunguka, na mifumo ya ikolojia hii sasa iko chini ya tishio la ukataji miti, kilimo na mabadiliko mengine katika matumizi ya ardhi na maendeleo ya haraka ya ukuaji wa mijini.”

Ameendelea kusema kuwa uvamizi unaoendelea zaidi katika makazi ya wanyama unaongeza fursa kwa virusi hatari kwa wanadamu kufanya mabadiliko kutoka kwa wanyama wao.

Kati ya mwaka 2030 na 2050, mabadiliko ya tabianchi yanatarajiwa kusababisha takriban vifo 250,000 vya ziada kwa mwaka kutokana na utapiamlo, malaria, kuhara na shinikizo la joto kali.

Pia amesema gharama za uharibifu wa moja kwa moja wa afya yaani, bila kujumuisha gharama katika sekta zinazoamua mustakbali wa afya kama vile kilimo na maji na usafi wa mazingira, inakadiriwa kuwa kati ya dola bilioni 2-4 kwa mwaka ifikapo 2030.

Kwa mujibu wa WHO ongezeko la halijoto duniani ambalo tayari limetokea linasababisha hali mbaya ya hewa ambayo huleta joto kali na ukame, mafuriko makubwa na vimbunga vinavyozidi kuwa na nguvu na pia dhoruba za kitropiki. Mchanganyiko wa mambo haya unamaanisha athari kwa afya ya binadamu inaongezeka na kuna uwezekano wa kuharakisha athari hizo.


342/