Main Title

source : Parstoday
Jumapili

28 Mei 2023

19:53:33
1369419

Rais wa Iran: Wanachama wa OPEC waungane kuzuia migawanyiko inayoibuliwa na Wamagharibi

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na Katibu Mkuu wa Shirika la Nchi Zinazouza Mafuta Kwa Wingi Duniani (OPEC) na kusema: "Nchi wanachama wa OPEC ziungane ili kuzuia njama za Wamagharibi za kuibua hitilafu katika shirika hilo."

Rais Raisi ameongeza kuwa: "Baadhi ya nchi za Magharibi zinataka kuleta mgawanyiko na hitilafu kati ya nchi wanachama wa OPEC, na hivyo wanachama wa OPEC wanapaswa kuzuia kufikiwa kwa malengo hayo kwa kuimarisha umoja."

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran Press, Rais wa Iran aliyasema hayo Jumamosi wakati wa kikao na Haitham Al Ghais, Katibu Mkuu wa OPEC. Raisi amesisitiza maingiliano chanya ya wanachama wa shirika hilo wao kwa wao kama jambo muhimu katika mafanikio ya shirika hilo la kimataifa na kuongeza: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa na ushirikiano amilifu na shirika hili na lengo la Iran ni kuendeleza na kuboresha kiwango na kuimarishwa ushirikiano huo.

Raisi amesema falsafa ya kuundwa OPEC ni kuunga mkono haki za wazalishaji wa mafuta na kuzuia ubaguzi dhidi yao na kusema: "OPEC katika kipindi kipya inaweza kudhibiti uchochezi na kuleta amani katika soko la mafuta."

Katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa OPEC Haitham Al Ghais amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ni miongoni mwa wanachama waanzilishi wa OPEC, daima imekuwa na ushirikiano wenye manufaa, madhubuti na amilifu na jumuiya hii na wanachama wake sambamba na kusistiza muungano wa wanachama wa OPEC."

Katibu Mkuu wa OPEC aidha ameelezea hali ya sasa ya soko la mafuta na kusema: "Tukiwa na umoja wa mawazo baina ya wanachama wa OPEC na kunufaika na uungaji mkono na ushirikiano wenye kujenga wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, tunaweza kuleta utulivu sokoni."

342/