Main Title

source : Parstoday
Jumatano

31 Mei 2023

13:58:56
1370147

Msimamo wa Kiongozi Muadhamu kuhusu kuhuishwa uhusiano wa Iran na Misri

Jumatatu ya jana tarehe 29 Mei, Sultan Haitham bin Tariq Aal Saeed wa Oman alikutana na kufanya mazungumzo hapa mjini Tehran na Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Katika mazungumzo hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliashiria matamshi ya Sultan Haitham bin Tariq Aal Saeed wa Oman kuhusu hamu na shauku ya Misri ya kufufuliwa uhusiano baina ya nchi hiyo na Iran na kueleza kwamba, "sisi tunakaribisha msimamo huu, na hatuoni tatizo katika (kufikiwa) hilo."

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesisitiza kuwa Iran inakaribisha azma ya kufufuliwa uhusiano wake na Misri.  Sultan wa Oman amefanya safari hapa nchini baada ya wiki iliyopita kufanya safari nchini Misri ambako alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Cairo akiwemo Rais Abdul-Fattah al-Sisi wa nchi hiyo. Safari ya kiduru ya Sultan wa Oman huko kaskazini mwa Afrika na kisha hapa Iran tangu awali ilizingatiwa na weledi wa mambo wa kieneo hususan wanaofuatilia masuala ya Iran na Misri. Hilo lilitokana na kuwa mstari wa mbele ufalme wa Oman katika diplomasia ya upatanishi hivyo ilikuwa ikitabiriwa kwamba, kuna uwezekano safari hiyo ikawa na lengo la kujadili suala la kuhuishwa uhusiano wa Iran na Misri hasa kwa kuzingatia matukio yaliyotokeza hivi karibuni katika eneo la Asia Magharibi.

Kuhusiana kadhia hiyo, maafisa wawili wa serikali ya Misri nao waliliambia gazeti la Imarati la The National kwamba, uhusiano wa Tehran na Cairo ni miongoni mwa mambo muhimu yaliyojadiliwa katika mazungumzo ya Sultan wa Oman na Rais Abdul-Fattah al-Sisi na kwa muktadha huo kuna uwezekano katika miezi michache ijayo, Iran na Misri zikabadilishana mabalozi.

Iran na Misri zikiwa nchi mbili za kimhimili katika ulimwengu wa Kiislamu zipo katika maeneo mawili nyeti na ya kimkakati. Hapana shaka kuwa, Misri na Iran ni mataifa mawili ambayo yanahesabiwa kuwa na utamaduni mkongwe ulimwenguni na tamaduni za mataifa haya mawili zilikuwa sababu yenye taathira kubwa na muhimu huko nyuma kama ambavyo hadi leo hali iko namna hiyo. Hata hivyo kumekuweko na matukio ya kisiasa ambayo daima yamekuwa sababu ya kukurubiana na kujitenga mataifa haya katika uhusiano wao.

Kujitenga na kuwa mbali kwa mara ya mwisho baina ya mataifa haya katika uhusiano kulianza 1979 Hijria Shamsia na hali hiyo ya utengano ingali inaendelea mpaka leo.

Katika siku hiyo ikiwa ni miezi mitatu tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu uhusiano wa kidiplomasia wa pande mbili ulikatwa baada ya Iran kulalamikia mkataba wa Cairo-Tel-Aviv mashuhuri kwa jina la mkataba wa amani wa Camp David. Ingawa mkataba huo ulipelekea Misri kutimuliwa katika Jumuiya yay Nchi za Kairabu, lakini Misri ikiwa na lengo la kuondokana na jinamizi la mgogoro ilimuunga mkono dikteta Saddam kwa hali na mali katika vita vya kulazimishwa Iran vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Baath wa Iraq.

Takribani miongo miwili baada ya kumalizika vita vya Iraq na Iran, Hosn Mubark Rais wa wakati huo wa Misri alikiri kwamba, askari 18,000 wa Misri walikuwa wakipigana bega kwa bega askari wa Baath wa Iraq dhidi ya Iran.

Pamoja na hayo, filihali eneo la Asia Magharibi linashuhudia matukio mapya ambayo yanaipa nguvu dhana ya kuweko ishara za kuimarishwa uhusiano wa Iran na Misri. Kutokana na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kulipa kipaumbele suala la kuimarisha uhusiano wa mataifa jirani na ya kieneo, hivi sasa kumepatikana matunda kama kurejeshwa tena uhusiano wa Iran na Saudi Arabia hatua ambayo imepokewa kwa mikono miwili na kupongezwa mno na akthari ya mataifa ya Kiarabu na Kiislamu ambayo yanaiona hatua hiyo kuwa ina taathira chanya katika kuimarisha usalama na uthabiti wa kieneo. Hapana shaka kuwa, mwenendo wa kuboreshwa uhusiano wa mataifa ya eneo, ukiwemo uhusiano wa Iran na Misri, mbali na kuwa na manufaa ya kiuchumi na kuongeza mashirikiano ya kisiasa na kiusalama, ni sababu muhimu ya kupatikana uthabiti wa kudumu kupitia mhimili wa kuwa na mitazamo mimoja mataifa ya eneo pasi na kutegemea uingiliaji wa kigeni katika masuala yao ya ndani.

Ndio maana Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akasema katika mazungumzo yake na Sultan wa Oman kwamba: Ana matumaini kwa kupanuliwa mawasiliano na ushirikiano baina ya serikali, umma wa Kiislamu utapata tena utukufu na adhama yake, na uwezo na suhula za mataifa ya Kiislamu kuwa kwa maslahi ya watu wote, mataifa na tawala za Kiislamu.

342/