Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

2 Juni 2023

21:08:26
1370717

Iran yakamata zaidi ya tani ya madawa ya kulevya kusini mashariki mwa nchi

Kamanda wa walinzi wa mpakani wa mkoa wa Sistan na Baluchistan wa kusini mashariki mwa Iran amesema kuwa, askari walioko chini ya amri yake wamefanikiwa kuangamiza magenge kadhaa ya magendo ya mihadarati na kukamata zaidi ya tani moja na kilo 370 za madawa ya kulevya.

Licha ya kuwa chini ya vikwazo vya makumi ya miaka, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran muda wote haijaacha kufanya jitihada za kupambana na mihadarati kiasi kwamba kila mwaka huwa inakamata zaidi ya tani elfu moja za madawa ya kulevya, kiwango ambacho ndicho kikubwa zaidi ya kukamatwa madawa hayo haramu ulimwenguni.

Vile vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko mstari wa mbele katika kuendesha operesheni za kupambana na madawa ya kulevya duniani na hadi hivi sasa zaidi ya askari wake 12,000 wameshauawa shahidi katika mapambano na madawa hayo. Ndio maana Umoja wa Mataifa umetangaza waziwazi kuwa Iran ndiye kiranja mkuu wa kupambana na mihadarati duniani.

Reza Shojaei, kamanda wa walinzi wa mpakani wa mkoa wa Sistan na Baluchistan huko kusini mashariki mwa Iran amesema leo Ijumaa wakati alipohojiwa na shirika la habari la IRNA kwamba, kumefanyika operesheni nane za kutumia silaha dhidi ya waendesha magendo ya madawa ya kulevya wiki iliyopita katika mpaka wa mkoa huo.

Ameongeza kuwa, askari wa Iran waliweka mitego ya masaa 24 ya usiku na mchana na kufanikiwa kukamata zaidi ya tani moja na kilo 370 za madawa mbalimbali ya kulevya katika mpaka wa mkoa huo. 

Waendeshaji wa magendo ya madawa ya kulevya yanayozalishwa katika nchi za Afghanistan na Pakistan, wanapenda kutumia njia ya Iran kwani ni ya mkato kuelekea barani Ulaya lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejitolea kikamilifu kupambana na magendo hayo.

342/