Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

12 Februari 2024

19:24:46
1437180

Kukiri Netanyahu kuweko mgogoro mkubwa wa kiuchumi Israel

Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni amekiri kwamba utawala dhalimu wa Israel umekumbwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi hivi sasa.

Netanyahu amesema hayo katika juhudi zake zilizofeli zamani za kujaribu kufifiliza hasara unazopata utawala wa Kizayuni kutokana na vita vya Ghaza lakini pamoja na hayo amelazimika kukiri kuwa, kuporomoka itibari ya Israel hivi sasa ni matunda ya vita vya Ghaza. Kituo cha Kizayuni cha Hayom kimesema kuwa, serikali ya Netanyahu imetumbukia kwenye kipindi kigumu sana ambacho utawala wa Kizayuni haujawahi kutumbukia ndani yake tangu mwaka 1995 na hii ni mara ya kwanza kwa itibari ya utawala wa Kizayuni kuporomoka kiasi chote hicho.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiwango cha hatari ya jeopolitiki dhidi ya utawala wa Kizayuni hususan hatari za kiusalama kwa kiwango cha muda wa kati na muda mrefu kimepanda hivi sasa. Zaidi ya hayo, kuna uwezekano baada ya kuanguka serikali ya Netanyahu, utawala wa Kizayuni wa Israel ukatumbukia kwenye machafuko makubwa ya kisiasa katika safu za Wazayuni wenyewe. 

Tangu baada ya kuanza operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa tarehe 7 Oktoba 2023, Netanyahu muda wote amekuwa akifanya njama za kufifiliza mafanikio makubwa ya wanamapambano wa Palestina katika kukabiliana na jeshi la Israel lililojizatiti kwa silaha kubwa za kisasa na amekuwa akidai kuwa eti ataendeleza vita hadi atakapoivunja nguvu HAMAS na kuuteka kikamilifu Ukanda wa Ghaza. Lakini matukio ya siku za hivi karibuni katika ardhi za Palestina yanaonesha kuwa, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni amefeli kufanikisha malengo yake haramu. Kushindwa baraza la mawaziri la Netanyahu kuibebeshwa HAMAS matakwa ya Wazayuni hususan suala zima la kubadilishana mateka, kushindwa jeshi la Israel kusimamisha mashambuizi ya wanamapambano wa Palestina huko Ghaza na kulazimika wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni kurudi nyuma, ni ushahidi mwingine wa kufeli siasa za Netanyahu katika siasa zake na kutofikia malengo aliyotangaza kuhusu kuanzisha vita huko Ghaza.

Migogoro ya kisiasa ndani ya utawala wa Kizayuni ni miongoni wa athari mbaya za siasa za kupenda vita utawala huo pandikizi. Mgogoro wa kiuchumi nao unazidi kuiandama Israel na kila kitu kinaonesha kuwa mgogoro huo wa kiuchumi utazidi kuwa mkubwa. Kushindwa Netanyahu kutatua matatizo ya ya kiuchumi, kumezidisha malalamiko ya Wazayuni ndani ya utawala wa Kizayuni. Familia za mateka wa Kizayuni walioko mikononi mwa makundi ya Palestina nazo zinazidi kuishinikiza serikali ya Netanyahu na hasa baada ya kufeli mazungumzo ya hivi karibuni ya kubadilishana mateka baina ya utawala wa Kizayuni na harakati ya HAMAS.Waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni ameshindwa pia kuvikinaisha vyama vya siasa ndani ya utawala wa Kizayuni ambavyo vimekataa kukubaliana na madai ya Netanyahu kuhusu mafanikio ya jeshi la Israel baada ya operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa. Netanyahu mwenyewe anajua vyema kwamba kumalizika vita vya Ghaza ni sawa na kumalizika maisha yake ya kisiasa na serikali yake na ni madhara makubwa pia kwa chama cha Likud. Kufanyika uchaguzi mpya katika hali tete iliyo nayo hivi sasa Israel na serikali ya Benjamin Netanyahu; ni mtihani mkubwa zaidi unaoukabili utawala wa Kizayuni. Mgogoro huu unaonekana ni mkubwa zaidi kuliko migogoro mingine iliyo nayo Israel hivi sasa. Baya zaidi ni kwamba hata vyama huru ndani ya bunge la utawala wa Kizayuni navyo havitoweza kutatua matatizo mengi iliyotumbukia ndani yake Israel hivi sasa. Kiujumla ni kuwa, siasa za kupenda vita za utawala wa Kizayuni zimeisababishia Israel matatizo mengi hasa ya kiuchumi na kiusalama na zimeutumbukiza utawala huo dhalimu katika mgogoro mkubwa ambao hata viongozi wenye misimamo mikali kama Benjamin Netanyahu wanalazimika kukiri kuweko migogoro hiyo na ndio maana wanafanya njama za kila namna za kujaribu kukhafifisha hali mbaya waliyo nayo Wazayuni na viongozi wao makatili.

342/