Main Title

source : Parstoday
Jumatano

17 Aprili 2024

17:10:09
1452134

Amir-Abdollahian: Mgogoro wa Asia Magharibi umesababishwa na mashambulizi ya Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan na kusisitiza kuwa, mgogoro uliopo katika eneo la Asia Magharibi hivi sasa umesababishwa na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni kwenye Ukanda wa Ghaza.

Katika mazungumzo hayo, Hosseim Amir Abdollahian amemueleza Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Bi Yōko Kamikawa kwamba, mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyofanywa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni yamefanyika kwa mujibu wa sheria za kimataifa, baada ya Israel kushambulia ubalozi wa Iran mjini Damascus Syria na kuua kigaidi maafisa kadhaa wa Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametilia mkazo pia wajibu wa kufanyika juhudi kubwa zaidi za kuulazimisha utawala wa Kizayuni usitishe jinai zake huko Ghaza kwani mgogoro wote uliopo kwenye eneo la Asia Magharibi umesababishwa na mashambulizi ya kikatili ya Israel kwenye ukanda huo.

Katika mazungumzo hayo ya simu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan ameelezea kusikitishwa mno na hali mbaya ya kibinadamu iliyosababishwa na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya wanawake, watoto wadogo, vizee na watu wa kawaida huko Ghaza na kusisitiza kuwa, kuna wajibu wa kufikishwa haraka misaada ya kibinadamu, kurejeshwa amani na utulivu na kuruhusiwa wakimbizi kurejea katika maeneo yao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan amelaani pia shambulio la Israel kwenye ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus Syria.

342/