Ismail Haniyah, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, na mmoja wa walinzi wake waliuawa shahidi Jumatano asubuhi (Julai 31) katika makazi yao mjini Tehran.
Mapema leo Alkhamisi asubuhi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesalisha umati mkubwa wa Waislamu waliojitokeza katika Swala ya Maiti ya Haniya na mlinzi wake. Swala hiyo ya Maiti imeswaliwa katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Tehran.
Kwa mujibu wa IRNA, Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Kiislamu ya Iran, katika hafla ya maziko ya Ismail Haniya sambamba na kutoa rambirambi za kuuawa shahidi mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas ameongeza kuwa, leo harakati za muqawama zimehatarisha falsafa ya kuwepo utawala wa Kizayuni ambapo walimwengu leo wanashuhudia kuelekea kuangamia utawala huo.
Akigusia operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa (Oktoba 7, 2023) na kuporomoka taratibu utawala wa Kizayuni na jinai zake katika Ukanda wa Gaza yakiwemo mauaji ya wanawake, watoto na raia, Qalibaf amesema kwa jinai hii, dunia inashuhudia makabiliano kati ya ubinadamu na watenda jinai.
Spika wa Bunge la Iran amesema mauaji ya makamanda wa muqawama huko Beirut na Tehran ni matokeo ya udhaifu wa utawala wa Kizayuni na kuongeza kuwa, mauaji na vitendo hivyo havitaathiri harakati za mhimili wa muqawama.
Akiashiria matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na kumalizika zama za kushambulia na kisha kukimbia, Qalibaf amefafanua kwamba Iran ina wajibu wa kujibu jinai hiyo (mauaji ya Ismail Haniyah) kwa wakati na mahala munasibu.
342/