24 Septemba 2024 - 16:21
Rais Pezeshkian atilia mkazo kuimairishwa uhusiano wa kiusalama baina ya Iran na Uturuki

Rais Masoud Pezeshkian amefanya mazungumzo na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kuimarisha uhusiano wake wa pande zote na Uturuki yakiwemo masuala ya usalama.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Rais Pezeshkian ameonana na Rais Erdogan mjini New York, Marekani alikokwenda kwa ajili ya Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, tunaamini kwamba, ushirikiano na kuaminiana pande mbili ndiyo siri wa ustawi na mafanikio yetu.

Amesema: Kama tutashikamana katika udugu wetu, utawala wa Kizayuni kamwe hautoweza kufanya jinai kama unazofanya hivi sasa huko Palestina, za kuua watoto na wanawake wasio na hatia na kushambulia maskuli, mahospitali na maeneo salama ya raia. Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya nazo zinaunga mkono jinai za Wazayuni ambazo zinafanywa mbele ya macho ya walimwengu.

Kwa upande wake, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema kuwa, zaidi ya miezi 11 imepita tangu utawala wa Kizayuni uanzishe mashambulizi ya kikatili na jinai za mauaji ya umati huko Ghaza na hilo linazidi kuthibitisha nia chafu ya Israel ya kuangamiza kikamilifu kizazi cha Wapalestina.

Amesema, kuimarishwa ushirikiano wa kiusalama baina ya Iran na Uturuki sambamba na ushirikiano katika nyuga nyingine hasa za kiuchumi, ni jambo la dharura sana.

342/