Lammy ameyasema hayo alipohutubia mkutano wa chama tawala cha Leba katika mji wa Liverpool, sambamba na kutilia mkazo kujitolea kwa Uingereza katika kuiunga mkono serikali ya Kiev. Amebainisha kuwa serikali ya London imejitolea kuipatia Ukraine msaada wa kijeshi wa pauni bilioni 3 (dola bilioni 3.99) kila mwaka "kwa muda mrefu kadiri itakavyohitajika."
Akinukuliwa na gazeti la The Guardian, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza amebainisha kuwa, ugumu na changamoto zinazotokana na mzozo wa Russia na Ukraine zinatazamiwa kuwa za "kina zaidi na kali zaidi" katika miaka ijayo.
Lammy amedai kuwa huu ni wakati muhimu kwa ajili ya kuonyeshwa ujasiri, uthabiti na uvumilivu kwa washirika wanaosimama bega kwa bega na Ukraine.
Matamshi ya waziri wa mambo ya nje wa Uingereza yanaonekana kuulenga msimamo wa utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden wa kutokuwa tayari kuiruhusu Ukraine itumie silaha zinazotolewa na nchi za Magharibi kwa mashambulizi ya masafa marefu katika eneo linalotambulika kimataifa kuwa ni la Russia.
Moscow imeonya kwamba kutoa ruhusa hiyo, ambayo kiongozi wa Ukraine Volodymyr Zelenskyyamekuwa akiiomba kwa miezi kadhaa, kutazifanya nchi za NATO ziwe washiriki wa moja kwa moja katika mzozo huo na kukabiliwa na jibu mwafaka la Russia.
Kuhusiana na wakati wa kukomesha vita baina yake na Ukraine, Russia haijawahi kuweka makataa na muhula maalumu, na imeshasema mara kadhaa kwamba operesheni yake ya kijeshi iliyoanza Februari 2022 itaendelea hadi malengo yake yatimie. Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alirudia tena msimamo huo siku ya Jumapili aliposema "hakuna njia mbadala ya ushindi wetu [wa Russia]".../
342/