Main Title

source : Pars Today
Jumatano

26 Juni 2019

08:29:42
955217

Mazungumzo ya Mkuu wa Jumuiya ya Mabunge ya Dunia mjini Tehran

"Mzizi wa matatizo mengi ya eneo la Mashariki ya Kati na dunia kwa ujumla ni udikteta wa baadhi ya nchi hususan Marekani ambayo inatekeleza sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na kukiuka sheria za kimataifa."

(ABNA24.com) "Mzizi wa matatizo mengi ya eneo la Mashariki ya Kati na dunia kwa ujumla ni udikteta wa baadhi ya nchi hususan Marekani ambayo inatekeleza sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na kukiuka sheria za kimataifa."

Hayo yamesemwa na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo yake na Gabriela Cuevas Barron, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabunge ya Dunia aliyeko safarini mjini Tehran. Ameongeza kuwa kuwepo kwa majeshi ya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na uingiliaji kati wake katika masuala ya ndani ya nchi mbalimbali ndiyo sababu ya matatizo na ukosefu  amani katika eneo hilo.

Amani na usalama ni suala linalohitajia ushirikiano lakini msingi wa siasa za Marekani ni kujichukulia maamuzi ya upande mmoja, suala ambalo linazuia kuwepo ushirikiano wa nchi za eneo hilo katika masuala ya usalama.

Akieleza umuhimu wa kadhia hiyo, Rais Hassan Rouhani ameashiria miaka 17 ya uingiliaji kati wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi za Afghanistan, Iraq, Syria na sasa Yemen na kusema: Usalama wa maeneo yote ya dunia ikiwemo Ghuba ya Uajemi, unapaswa kulindwa na nchi za eneo husika.  

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema katika mazungumzo yake na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabunge ya Dunia kwamba kuna udharura wa kutumia uwezo wa mabunge kwa ajili ya kupunguza migogoro ya kikanda na kuendeleza miradi na mipango ya kuimarisha ushirikiano wa kieneo. 

Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita nchi za Mashariki ya Kati zimepita katika kipindi kigumu na chenye misukosuko mingi na zimekumbana na mashinikizo na migogoro iliyosababishwa na sera za nchi zinazopenda kuingia mambo ya ndani ya nchi nyingine. Hali hiyo iliipa Marekani fursa ya kutekeleza siasa zake za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja katika masuala ya kimataifa. Hatua ya Marekani ya kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambayo yaliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kupuuza sheria za kimataifa ambazo ndizo zinazolinda usalama na amani ya kimataifa ni matokeo ya mienendo kama hiyo na serikali ya Washington na washirika wake. Inasikitisha kuona kwamba, baadhi ya tawala za eneo la Ghuba ya Uajemi kama Saudi Arabia na Imarati zimejiunga na siasa za serikali ya Washington za kuzusha migogoro na kueneza shari kutokana na mfungamano wao mkubwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Matamshi yaliyotolewa na Rais Hassan Rouhani katika mazungumzo yake na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabunge ya Dunia yanaashiria uhakika huu. Rais Rouhani ameashiria uchokozi uliofanywa na Marekani wa kutuma ndege isiyo na rubani katika anga ya Iran na kusema: "Hatua hiyo ni harakati ya Washington za kuanzisha mivutano mpya katika eneo la Mashariki ya Kati na kuhatarisha amani ya njia kuu ya majini ya Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman. Taasisi zote za kimataifa zinapaswa kutoa jibu linalofaa kwa uchokozi huu wa Marekani."  

Swali linalojitokeza hapa ni kwamba, ni kwa kiwango gani taasisi za kimataifa zinaweza kusaidia kuondoa changamoto hizi? Na je, Jumuiya ya Mabunge ya Dunia ambayo inaakisi mitazamo ya mataifa mbalimbali ya dunia inaweza kutoa njia mwafaka ya utatuzi na kutayarisha mazingira bora zaidi ya ushirikiano wa mataifa hayo katika kukabiliana na vitisho? 

Kazem Jalali ambaye ni mwakilishi katika Bunge la Iran na mkuu wa Kituo cha Utafiti cha Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu anasema: "Jumuiya ya Mabunge ya Dunia ina nafasi muhimu sana katika dunia ya sasa. Mabunge yana uhusiano wa karibu na matakwa ya mataifa ya nchi mbalimbali yanaweza kuakisi matakwa na mitazamo ya watu wa mataifa hayo. Kwa msingi huo Jumuiya ya Mabunge ya Dunia, kama lilivyo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ni fursa nzuri inayoweza kutumiwa kwa ajili ya kujadili na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa." 

Jumuiya ya Mabunge ya Dunia ambayo ilianzishwa zaidi ya miaka 110 iliyopita na ina wanachama karibu 180 ni medani ya mawasiliano na ushirikiano baina ya wawakilishi wa mataifa mbalimbali na moja kati ya malengo makuu ya kuanzishwa kwake ni kusaidia jitihada za kuimarisha amani na ushirikiano baina ya mataifa kupitia njia ya mazungumzo baina ya mabunge ya dunia. Kwa msingi huo jumuiya hiyo ina taathira kubwa katika upeo wa kimataifa na sambamba na kuyaunganisha pamoja mabunge ya nchi mbalimbali, inaweza pia kukurubisha pamoja mitazamo mkabala wa vitisho na kusaidia kubaini sababu zinazovuruga na kuhatarisha usalama na amani duniani.