(ABNA24.com) Rais Rouhani alisema hayo jana Jumapili katika mazungumzo yake na Alexander Schallenberg, Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria na kuongeza kuwa, nchi za Ulaya zinapaswa kusimama kidete dhidi ya hatua za Marekani zinazokiuka sheria.
Amesema, "tunaamini makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yanaweza kuokolewa. Mapatano hayo si ya Iran au nchi za Ulaya pekee, bali yanaweza kuwa na mchango mkubwa kwa amani na usalama wa eneo na dunia kwa ujumla."
Amesema Iran kwa upande wake imefungamana na JCPOA na kusisitiza kuwa, makubaliano hayo yanaweza kutumiwa kama msingi wa kuunda muamana mpya kati ya Iran na nchi za Magharibi ikiwemo Marekani na Umoja wa Ulaya.
Dakta Rouhani ameeleza bayana kuwa, EU inapaswa kutekeleza wajibu wake wa kibinadamu dhidi ya ugaidi wa Marekani wa kuliwekea taifa hili vikwazo vya chakula na dawa.
Hali kadhalika Rais Hassan Rouhani amegusia kuhusu uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Vienna na kubainisha kuwa, "nchi mbili hizi zina fursa nzuri ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili haswa katika nyuga za uchumi. Tunatumai Austria itapuuza mashinikizo ya Marekani ya kuzitaka nchi za dunia zisiwe na uhusiano na Iran."
Kwa upande wake, Alexander Schallenberg, Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria mbali na kusisitiza haja ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga za uchumi na biashara, ameutaja mpango wa "Ubunifu wa Amani ya Hormuz" uliopendekezwa na Iran, kama ramani ya njia ya kupatikana uthabiti, amani na usalama wa kudumu katika eneo zima la Asia Magharibi.
Kadhalika amesema kuinusuru JCPOA ni sera kuu ya serikali ya Vienna na Umoja wa Ulaya na kwamba nchi hizo za EU zitafanya juu chini kuhakikisha kuwa mapatano hayo yanabakia hai.
.............
340