28 Aprili 2020 - 12:33
Zarif: Baada ya kufeli "mashinikizo ya kiwango cha juu" Pompeo anataka kuwa mshirika katika JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, uamuzi wa Marekani wa kutaka kurejea katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni matokeo ya kufeli na kushindwa vibaya siasa za "mashinikizo ya kiwango cha juu" dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

(ABNA24.com) Muhammad Javad Zarif amesema katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Miaka miwili iliyopita, Mike Pompeo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani na Rais wake walitoa tangazo la kusitishwa ushiriki wa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA wakidhani kwamba, mashinikizo yao ya kiwango cha juu yataipigisha magoti Iran. Zarif amesema, baada ya kushindwa vibaya na kwa fedheha mashinikizo hayo ya kiwango cha juu sasa Pompeo anataka kuwa mshirika katika makubaliano ya JCPOA. Zarif amewaambia viongozi wa Marekani kwamba: "Acheni njozi zenu, taifa la Iran daima limekuwa likijiamulia mambo yake lnyewe."

Jumapili ya jana gazeti la New York Times liliripoti kuwa, Marekani inafanya jitihada za kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Iran ambavyo kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA vitafutwa tarehe 18 mwezi Oktoba mwaka huu.

Gazeti hilo limefichua kwamba, ili kuweza kutekeleza stratijia yake, Mike Pompeo amebuni mpango ambao kwa mujibu wake Marekani inadai kuwa, katika mtazamo wa sheria hadi sasa ni mshirika katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. New York Times limeandika kuwa kwa hakika lengo halisi la mpango huo ni kurejesha vikwazo vya silaha vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vilivyowekwa mwaka 2006 na 2007 vilivyopiga marufuku kuuzwa na kuingizwa silaha nchini Iran.

Baada ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ilipangwa kuwa vikwazo hivyo vitaondolewa tarehe 18 Oktoba mwaka 2020 baada ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuthibitisha kwamba miradi ya kuzakisha nishati ya nyuklia nchini Iran inafanyika kwa malengo ya amani. 

..............
340