Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mkuu wa Mashtaka wa Uturuki ameitaka Interpol imkamate Dahlan kwa tuhuma za ujasusi na kushiriki katika jaribio lililofeli la mapinduzi ya kijeshi la kutaka kuiondoa madarakani serikali ya nchi hiyo lililofanyika Julai 15, 2016.
Muda mfupi baada ya jaribio hilo la mapinduzi, na kwa kutegemea ushahidi wa ungamo la makosa uliotolewa na majasusi wawili wa Imarati, serikali ya Uturuki iliutuhumu utawala wa kifalme wa Abu Dhabi kwamba uliwapatia suhula na msaada wa fedha watu walioratibu mpango wa kuiangusha serikali hiyo. Kwa mujibu wa nyaraka zilizotolewa na Uturuki, serikali ya Imarati, kupitia Mohmmed Dahlan mshauri wa mrithi wa ufalme wa nchi hiyo iliupatia mrengo wa Fethullah Gülen na baadhi ya maafisa waandamizi wa jeshi la Uturuki fedha taslimu dola bilioni tatu. Huko nyuma na kabla ya hapo, Dahlan alikuwa mwanachama mwandamizi wa harakati ya Fat-h ya Palestina, lakini alikamatwa na askari wa Israel na kufungwa jela wakati wa harakati zake za mapambano kupitia kundi hilo. Katika kipindi cha mwaka mmoja alipokuwa jela, Mohammed Dahlan alianza kulitumikia shirika la ujasusi la Israel Mossad, ambapo kwa kupitia njia hiyo alitoa huduma kubwa kwa utawala wa Kizayuni. Mbali na kushiriki katika mauaji ya kiongozi wa zamani wa Fat-h na Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO, Yasir Arafat, kwa miaka kadhaa Mohammed Dahlan amewafanyia uhaini na usaliti wanamapambano wenzake wa Palestina. Baada ya kufichuka uhaini wake na kutambulika kuwa ni jasusi, Dahlan alitoroka Palestina na kukimbilia Imarati alikoanzisha makazi yake mapya. Hivi sasa Mohammed Dahlan ni mshauri wa mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Mohammed bin Zayed Al Nahyan huko Abu Dhabi. Mbali na kutumiwa kama kiunganishi baina ya Montenegro, Serbia na utawala wa Imarati, haini huyo wa Palestina anahusika pia kuunganisha harakti za jenerali muasi wa Libya Khalifa Haftar na utawala wa Abu Dhabi. Hivi karibuni, Mohammed Dahlan alijikurubisha na wanasiasa wa Tunisia na akawapendekezea kuwapatia fedha na misaada mingine mkabala wa kukomesha harakati na shughuli za chama chenye mielekeo ya Kiislamu cha nchi hiyo cha An-Nahdhah.
Kutokana na harakati nyingi zilizoendeshwa na serikali ya Abu Dhabi kwa msaada wa Mohammed Dahlan, serikali ya Uturuki imeamua hatimaye kuvunja kimya chake cha miezi kadhaa kwa kuliibua fali la jasusi huyo wa utawala wa Kizayuni, na kwa kufanya hivyo, kuuingiza kwenye awamu nyingine mpya mvutano na msuguano uliopo kati yake na serikali ya Imarati.
Lakini mbali na kadhia ya Dahlan, katika miaka ya karibuni Uturuki na Imarati zimekuwa zikivutana na kusuguana kila mara juu ya masuala kadhaa ya kieneo. Mvutano baina ya pande mbili ulioanza miaka kadhaa nyuma juu ya kadhia ya Ikhwanul Muslimin ya Misri, jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali Erdogan, uwepo wa pande hizo mbili barani Afrika, mgogoro wa Qatar na baadhi ya nchi za Kiarabu na mapinduzi ya kijeshi ya Misri yaliyoindoa madarakani serikali ya kwanza ya kidemokrasia ya marehemu Mohammad Morsi, umetambaa hadi kwenye kadhia inayoendelea hivi sasa ya mgogoro wa Libya.
Libya imegeuka uwanja wa kutunishiana zaidi misuli nchi hizo mbili, ambazo kila moja inaunga mkono moja ya pande mbili kuu hasimu kwa madhumuni ya kuimarisha zaidi satua na ushawishi wake katika nchi hiyo ya Kiafrika; na kwa njia hiyo kuweza kunufaika kiuchumi na utajiri wake hasa wa mafuta. Kuhusiana na nukta hiyo, Profesa Changiz Tumar, mtaalamu wa masuala ya Asia Magharibi na mkuu wa chuo kikuu cha Ahmet Yesevi cha Kazakhstan anasema: "Mbali na Saudi Arabia, uhusiano wa nchi mbili za Uturuki na Imarati kila mara umekuwa ukiambatana na mivutano na tofauti, kwa kila upande kutaka kumtunishia misuli mwenzake na kutaka kushika nafasi ya uongozi katika eneo."
Ukweli wa mambo ni kuwa, ushindani wa kieneo baina ya Ankara na Abu Dhabi kwa upande mmoja, na kadhia iliyoshindikana hadi sasa kupatiwa suluhisho ya vita vya ndani na vya niaba ya Libya kwa upande mwingine, vimegubika uhusiano wa kisiasa wa nchi hizo mbili. Na hata kama mvutano kati ya Uturuki na Imarati una sura ya kisiasa na kiusalama, lakini taathira yake inashuhudiwa wazi kwenye uhusiano wa kiuchumi pia wa pande hizo mbili, kiasi kwamba kuanzia mwaka 2018 na kuendelea, kiwango cha mabadilishano yao ya kibiashara kimepungua sana. Itakumbukwa kuwa mabadilishano ya kibiashara kati ya Uturuki na Imarati ambayo mnamo mwaka 2015 yalikuwa ya kiwango cha takriban dola bilioni saba, yaliongezeka hadi dola bilioni 15 katika mwaka 2017. Lakini kuanzia mwaka 2018 kiwango hicho kilipungua hadi chini ya dola bilioni saba na kuanzia mwaka 2019 hadi miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu wa 2020 yamepungua zaidi ya kiwango hicho.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa: Kutokana na kushadidi tofauti kati ya Uturuki na Imarati katika masuala mbalimbali, ni wazi kwamba hatua ya Ankara ya kutaka kulipa sura ya kimataifa faili la ujasusi la Mohammed Dahlan, mshauri wa mrithi wa ufalme wa Abu Dhabi inaweza kuzifikisha mahala pabaya zaidi tofauti baina ya pande hizo mbili na hata kuwa chanzo cha kushadidi moto wa vita kati ya pande mbili hasimu nchini Libya.../
342/