Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kila mwaka mji wa Basra umekuwa ukishuhudia machafuko katika msimu wa kiangazi; machafuko ya kupinga serikali ambayo kila mwaka huambatana na mauaji na umwagaji wa damu. Kwa miaka mingi sasa Iraq imekumbwa na matatizo mengi kama vile ukosefu wa ajira na huduma mbovu za kijamii hasa kukatika ovyo umeme na kukosekana maji safi ya kunywa. Kama ambavyo hatuwezi kuilaumu serikali iliyopita ya Waziri Mkuu Adil Abdul Mahdi ambayo ilitawala Iraq kwa muda wa mwaka mmoja tu, hatuwezi kuilaumu pia serikali ya hivi sasa ya Iraq ya Waziri Mkuu Mustafa al Kadhimi kwani ndio kwanza imeingia madarakani. Ukweli ni kuwa matatizo makubwa ya Iraq yakiwemo ya mji wa Basra, ni matunda ya utawala mbovu na wa kidikteta wa chama cha Baath na uvamizi wa Marekani ambao umewasababishia matatizo makubwa wananchi wa Iraq.
Pamoja na hayo yote, lakini hivi sasa kuna masuala mawili mengine makuu yanayowatesa wananchi wa Iraq nayo ni ufisadi na kuuliwa kigaidi wanaharakati wa masuala ya kijamii. Tangu mwaka 2003 wakati ulipoanguka utawala wa Baath huko Iraq hadi hivi sasa, yaani katika kipindi cha miaka 17, kumefanyika ufisadi na ubadhirifu mkubwa nchini Iraq unaokadiriwa kufikia dola bilioni 400 za Kimarekani, suala ambalo hakuna raia yeyote anayeweza kukubaliana nalo. Ufisadi mkubwa kiasi hicho ndio ulioepelekea kukosekana huduma muhimu na za kimsingi kwa raia kama umeme, maji safi ya kunywa na uchakavu wa miundombinu. Moja ya sababu za kutokea machafuko ya kila mwaka mjini Basra Iraq ni kwamba, licha ya nchi hiyo kuwa na utajiri mkubwa hususan mji wa bandari wa Basra, lakini migogoro mikubwa kama ya ukosefu wa ajira na kutokuwepo huduma za kimsingi kabisa za kijamii inaendelea kuwatesa wananchi wa Iraq. Kila siku ya Mungu, mapipa milioni 3 na laki tano ya mafuta ghafi ya Basra yanasafirishwa nje ya Iraq lakini wananchi wa mkoa huo ambao asilimia karibu yote ni Waislamu wa Kishia hawafaidiki na utajiri wa mkoa wao.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, hali iliyopo hivi sasa huko Basra Iraq, imeletwa kwa makusudi na watu wenye chuki na wananchi wa Iraq. Qais al Khaz'ali, Katibu Mkuu wa harakati ya Aswaib Ahlul Haq ya Iraq anaamini kuwa, hali ya hivi sasa ya Basra ina malengo ya kisiasa na kuna watu wenye ushawishi ndio wanaoshikilia kuwepo hali hiyo. Naye Nouri al Maliki, Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq amesema, matukio ya Iraq yana malengo ya kisiasa. Wachambuzi wengine wa mambo wanasema kuwa, kuna malengo mawili makuu ya kisiasa katika matukio hayo ya Basra, huko Iraq.
Shabaha ya kwanza ya matukio hayo kwa mujibu wa wachambuzi hao wa mambo, ni kumuondoa madarakani Mkuu wa Mkoa wa Basra, Asa'ad Abdul Ameer al Eidani ambaye anapingwa vikali na Saudi Arabia kiasi kwamba hivi sasa televisheni za Saudia za al Hadath na al Arabiyyah zinaendesha propaganda kubwa ya kumbebesha lawama zote al Eidani. Itakumbukwa kuwa mwezi Februari 2019 al Eidani aliilaumu Marekani kwa kuiwekea vikwazo Iran suala ambalo liliihamakisha Washington na vibaraka wake hasa Saudi Arabia. Gavana huyo wa Basra alisema, mkoa huo kamwe hauwezi kutumika kama wenzo wa kufanikishia vikiwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Lengo la pili la machafuko ya Basra ni kujaribu kuifikia na kuivunja jela kubwa ambayo wamefungwa huko viongozi mbalimbali wa chama cha Baath na magaidi wakubwa wanaoungwa mkono na Saudi Arabia.
342/