5 Novemba 2020 - 12:22
Kujiondoa rasmi Marekani katika Mapatano ya Tabianchi ya Paris

Marekani ambayo imejiondoa katika mikataba kadhaa ya kimataifa wakati wa utawala wa Donald Trump, sasa imejiondoa rasmi katika Makubaliano ya Mabadiliko ya Tabianchi yaliyofikiwa mjini Paris, Ufaransa mwaka 2015. Mapatano hayo ni muhimu katika kulinda mazingira ili kuzuia ongezeko la joto duniani.

hirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Jana Novemba nne Marekani ilitangaza rasmi kujiondoa katika Mapatano ya Kimataifa ya Tabianchi na hivyo kukamilisha mchakato ulioanza mwaka mwaka 2017 wakati Trump alipotangaza nia ya nchi yake ya kujiondoa katika mapatano hayo. Trump alidai kuwa mapatano hayo ya kimataifa ya kulinda mazingira yatasababisha hasara kwa mashirika na walipa kodi wa Marekani. Aidha Trump alisisitiza kuwa, nchi yake iko tayari kurejea katika mapatano hayo iwapo yatabadilishwa kama inavyotaka Marekani. Katika kipindi cha miaka mitatu sasa Trump amekuwa akitumia kila fursa kuyashambulia mapatano hayo.

Mapatano ya Tabianchi ya Paris yalifikiwa katika fremu ya Kongamano la Mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCC) kwa lengo la kupunguza utoaji wa gesi zinachochafua mazingira ambazo aghalabu hutoka katika viwanda. Gesi hizo hupelekea kuwepo mabadiliko katika tabianchi na hasa husababisha ongezeko la joto duniani. Nchi 197 ziliidhinisha mapatano hayo tarehe 12 mwezi Disemba mwaka 2015 mjini Paris.

Marekani ambayo inadai kuwa ni dola kubwa lenye nguvu duniani ni mpinzani mkubwa zaidi wa hatua chanya za kukabiliana na ongezeko la joto duniani. Trump ametangaza bayana kuwa haamini hata kidogo kadhia ya mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la joto duniani. Kwa msingi huo, Marekani ambayo yenyewe ni kati ya wachafuzi wakubwa zaidi wa mazingira duniani, imekataa kushiriki katika hatua za kuzuia ongezeko la joto duniani.

342/