22 Novemba 2020 - 12:16
Bobi Wine: Rais Museveni anakabiliwa na kizazi chenye hasira na njaa

Mgombea urais wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine amesema kuwa, Rais Yoweri Museveni wa nchi hiyo anakabiliana na kizazi ambacho kitafanya kila iwezelo kupigania uhuru.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mwanasiasa huyo chipukizi amesema hayo katika hafla ya maombi iliyoandaliwa katika makao makuu ya chama chake kuwaombea watu waliouawa katika maandamano ya siku mbili yaliyokumba Uganda, siku moja baada ya kuachiwa kutoka kizuizini.

Akimlenga moja kwa moja kiongozi wa nchi moja kwa moja Bobi Wine amesema Bwana Museveni anakabiliwa na kizazi ambacho kina njaa na hasira kwa wakati mmoja.

Kiongozi huyo wa upinzanii ambaye amekuwa akitiwa mbaroni mara kwa mara amesisitiza kuwa, hakuna kiwango chochote cha mabomu ya machozi au mateso ambacho kitawaogopesha na kuwafanya waachane na njia waliyoichagua ya kupigania haki.

Akizuungumzia matukio ya hivi karibuni nchini Uganda, Bobi Wine amesema kuwa, mashambulio yaliyofanywa dhidi ya raia wiki hii yameweka wazi udhalimu wa serikali ya sasa iliyo madarakani.

Amesisitiza pia kwamba, damu ya raia wasiokuwa na hatia iliyomwagika wiki hii haitaenda bure, na kuongeza kuwa haki itatekelezwa.

Bobi Wine aliachiwa kwa dhamana siku ya Ijumaa, baada ya kushtakiwa kwa kukiuka kanuni za kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona. na atakabiliwa na kifungo cha hadi miaka saba gerezani akipatikana na hatia.

Ripoti zinasema kuwa, watu wasiopungua 68 wameuawa katika maandamano yaliyoambatana na vurugu ambayo yalianza Jumatano ya wiki hii mjini Kampala mara tu mwanasiasa kijana Bobi Wine kutiwa mbaroni na vyombo vya usalama akiwa katika kampeni zakke za uchaguzi. Hata hivyo takwimu za polisi zinasema ni watu 28 ndio waliouawa katika machafuko hayo.

342/