27 Januari 2021 - 11:38
Takht Ravanchi: Utapeli ndio msingi mkuu wa siasa za mambo ya nje za Israel

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, utapeli na kujionesha kuwa ni watu waliodhulumiwa, ndio msingi mkuu wa siasa za mambo ya nje za utawala wa Kizayuni akisisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ina haki ya kujihami mbele ya vitisho vya utawala huo pandikizi.

Majid Takht Ravanchi alisema hayo jana Jumanne katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichozungumzia kadhia ya Palestina na ambacho kimefanyika kwa njia ya Intaneti na kuongeza kuwa, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita utawala dhalimu wa Israel umevunja mtawaliwa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama linalohusu makubaliano ya JCPOA.

Amesema, katika kipindi chote hicho, utawala wa Kizayuni haukuacha fursa yoyote ila umeitumia kwa ajili ya kuyaangamiza mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kusisitiza kuwa, utapeli, udanganyifu na kujionesha ni watu waliodhulumiwa, ndio msingi mkuu wa siasa za mambo ya nje za Israel.

Mwakilishi huyo wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa aidha amesema, Wazayuni wanatumia utapeli na udanganyifu huo kuficha dhulma na jinai zisizo na kifani wanazowafanyia Wapalestina na fitna na uchochezi wanaoufanya katika eneo hili, hivyo Baraza la Usalama linapaswa kuwa macho mbele ya nia mbaya na uongo unaoenezwa na utawala katili wa Israel.

Amesema, ni haki ya Iran kujihami na kujibu vitisho na chokochoko zozote inazofanyiwa kama vile vitisho vilivyotolewa jana na mwakilishi wa Israel katika Umoja wa Mataifa ambavyo ni uvunjaji wa wazi wa kifungu nambari mbili cha umoja huo na tab'an Baraza la Usalama nalo linapaswa kuuchukulia hatua za kinidhamu utawala wa Kizayuni kwa vitisho vyake hivyo.

342/