25 Machi 2021 - 11:03
Haki za binadamu; chombo cha kisiasa cha nchi za Magharibi katika kukabiliana na Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa azimio lililopitishwa hivi karibuni na baadhi ya nchi za Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kikao cha 46 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, halina itibari yoyote ya kisheria na wala halikubaliki kimataifa.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema jana Jumatano kwamba, azimio la Baraza la Haki za Binadamu dhidi ya Iran limepitishwa kwa kura chache mno katika hali ambayo ripota maalumu wa baraza hilo anayeshughulikia masuala ya Iran amekataa kwa makusudi kuashiria maafa yanayowapata makumi ya watoto wa Iran wasio na hatia na vilevile mamia ya wagonjwa wanaotaabika kutokana na ugumu wa kupata dawa na vifaa vinavyohitajika vya matibabu, kutokana na vikwazo vya kudhalimu ilivyowekewa na nchi za Magharibi.

Azimio hilo lililopasishwa kwa kura 21 za ndio, 12 za hapana na 14 ambazo hazikuunga mkono upande wowote, ni azimio lile lile lililopasishwa mwaka uliopita kwa lengo la kurefusha muda wa ripota huyo maalumu wa Baraza la Haki za Binadamu.

Kuna mgongano wa wazi katika misimamo iliyotangazwa rasmi na nchi zilizounga mkono azimio hilo dhidi ya Iran katika Baraza la Haki za Binadamu na matendo yao, na suala hilo linathibitisha kwamba nchi za Magharibi zinatumia suala la haki za binadamu kama chombo cha kisiasa katika kuamiliana na Iran.

Ukiukaji wa wazi wa nchi hizo kuhusu suala zima la haki ya kulinda uhai na haki ya kudhaminiwa dawa na matibabu maelfu ya raia wa Iran na hasa katika kilele cha janga la corona kutokana na vikwazo vikali na vya pande zote vya Marekani, na muhimu kuliko yote, ushirikiano wa baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani katika kutekeleza vikwazo hivyo dhidi ya Iran, unazifanya nchi hizo zisifae kabisa kudai kuwa ni watetezi wa haki za binadamu duniani.

Katika muongo mmoja uliopita, baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama la Haki za Binadamu wamekuwa wakitoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran na kuunga mkono kisiasa ripoti zote za ripota maalumu wa baraza hilo katika hali ambayo, nchi hizo zinapasa kuwajibishwa kuhusiana na ukiukaji wao wa haki za binadamu za watu wa Iran, badala ya kujipa fursa ya kuwa mshataki na jaji kwa wakati mmoja.

Azimio la Baraza la Haki za Binadmu limepitishwa dhidi ya Iran katika hali ambayo hatua ya baadhi ya nchi za Ulaya zilizounga mkono azimio hilo la kisiasa ni miongoni mwa wakiukaji wakubwa wa haki za binadamu duniani kutokana na hatua zao za kushirikiana na Marekani katika kuiwekea Iran vikwazo vya dawa na uchumi, kuunga mkono na kuwapa hifadhi magaidi wakubwa waliohusika na mauaji ya raia wa Iran na vile vile kuiuzia Saudi Arabia silaha hatari mbazo zinatumika kuwaua kinyama watu wa Yemen, na hasa wanawake na watoto.

Katika uwanja huo, Ismail, Baqai Hamaneh, mwakilishi wa Iran katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi anasema: Baadhi ya nchi kama Uingereza, Marekani, Ufaransa, Ujeruman na Canada zinatumia suala la haki za binadamu kwa ajili ya kukabiliana kisiasa na nchi pinzani na wakati huo huo kushiriki moja kwa moja katika mauaji ya watu wa Yemen wasio na hatia kwa kuiuzia silaha Saudia.

Nchi za Magharibi zinatumia vibaya na kisiasa suala la haki za binadamu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika hali ambayo Iran kwa mujibu wa mafundisho yake ya kidini, katiba, sheria zake nyingine za kawaida na sheria za kimataifa inafanya juhudi kubwa za kuimarisha haki za binadamu.

Kupitishswa kisiasa tena kwa kura chache mno, azimio la kukaririwa dhidi ya Iran katika Baraza la Haki za Binadamu kunathibitisha wazi kwamba hatua ya kipropaganda na kimaonyesha ya baadhi ya nchi za Magharibi dhidi ya Iran, haina uungaji mkono wowote katika ngazi za kimataifa na rekodi nyeusi ya nchi hizo kuhusiana na suala zima la haki za binadamu haiwezi kuwa kipimo kinachofaa cha kutathmini hali ya haki za binadamu katika nchi huru zinazojitawala kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

342/