10 Julai 2021 - 12:42
Joseph Lambert ateuliwa kuwa Rais wa muda wa Haiti

Mkuu wa Baaraza la Seneti la Haiti Joseph Lambert ameteuliwa kuwa Rais wa muda wa nchi hiyo siku chache baada ya mauaji ya kutisha dhidi ya Rais wa nchi Jovenel Moise.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Wajumbe wa Baraza la Seneti la Haiti wamemchagua kwa kura nyingi Joseph Lambert na kumpa jukumu la kuiongoza kwa muda nchi hiyo na anatarajiwa kuapishwa ili aanze kuiongoza rasmi nchi hiyo katika kipindi cha mpito.

Vyombo mbalimbali vya habari Jumatano iliyopita vilimnukuu Waziri Mkuu wa Haiti, Claude Joseph akithibitisha kutokea shambulio na mauaji dhidi ya Rais Jovenel Moïse na kusema kuwa limefanywa na makomandoo waliokuwa na silaha kwa kusaidiwa na mamluki kutoka nje ya Haiti.

Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama na mataifa mbalimbali yametoa taarifa yakilaani mauaji dhidi ya Rais Jovenel Moise wa Haiti, aliyeuawa Jumatano iliyopita kwa kupigwa risasi katika mji mkuu wa nchi hiyo Port-au-Prince.

Rais Jovenel Moïse amekuwa madarakani tangu mwezi Februari mwaka 2017 na aliingia uongozini kufuatia uchaguzi uliotokana na mtangulizi wake Michel Martelly kujiuzulu.

Tayari watu 17 wametiwa mbaroni wakishukiwa kuhusika na mauaji ya rais wa Haiti Jovenel Moïse siku ya Jumatano.

Maafisa wa serikali ya Haiti wanasema kuwa, washukiwa wawili wana uraia wa Marekani na Haiti, huku wengine wakiwa ni raia wa Colombia.

Serikali ya Colombia imesema miongoni mwa washukiwa  waliotiwa mbaroni, sita  walihudumu kama maafisa wa jeshi la nchi hiyo.

342/