Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Akizungumza leo Jumatano, Stephane Dujarric, Msemaji wa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema juhudi zozote zinazovuruga mwenendo wa kisiasa wa mpito nchini Sudan bila shaka unahatarisha maendeleo yaliyofikiwa katika uwanja huo na pia katika sekta ya uchumi.
Amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitaka pande zote nchini Sudan kufungamana na malengo ya watu wa nchi hiyo ya kutaka kuwa na mustakbali jumuishi, wenye amani na unaozingatia misingi ya demokrasia na uthabiti nchini.
Televisheni ya taifa ya Sudan jana iliripoti kuhusu jaribio la mapinduzi lililofanywa na wafuasi wa Omar al-Bashir, rais wa zamani wa nchi hiyo jeshini. Katika radiamali yao, viongozi wa sasa wa Sudan wamewataka wananchi kuwa macho na kuvunja njama zozote za kutaka kuleta vurugu nchini. Wamewataka wafanye kila linalowezekana kwa ajili ya kulinda nchi yao
Picha za karibuni mitandaoni zinaonyesha vifaru na magari ya kijeshi yakiwa mitaani katika miji kadhaa ya nchi hiyo kufuatia jaribio hilo la mapinduzi.
Afisa mmoja wa kijeshi amesema tayari maafisa 40 wa jeshi wametiwa nguvuni kwa tuhuma za kushiriki katika jaribio hilo lililofeli la mapinduzi.
Jeshi la Sudan limetoa taarifa likielezea kushindwa jaribio hilo na kuwataka raia wa nchi hiyo wakabiliane na wahusika wa jaribio hilo la mapinduzi.
342/