9 Machi 2022 - 11:42
Umoja wa Mataifa wahimiza kuthaminiwa mchango wa wanawake katika maendeleo

Umoja wa Mataifa umehimiza kuthaminiwa mchango wa wanawake na kuwajumuisha katika kila nyanja ili kutimiza ajenda ya maendeleo endelevu na kukabiliana na changamoto zingine zikiwemo za janga la COVID-19 na mabadiliko ya tabianchi.

Wito huo umetolewa katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake  iliyoadhimishwa kote ulimwenguni hapo jana Machi 8.

Sima Bahous, mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake amesema kuwa, pamoja na mchango wao mkubwa, wanawake kote duniani wanaendelea kukabiliwa na changamoto nyingi ambapo kwa mfano hivi sasa nchini Ukraine kunashuhudiwa hali ya kuogofya ambako athari za vita kwa wanawake na wasichana wakiwemo maelfu ya watu waliotawanywa ni ukumbusho kwetu sote kwamba “Vita vyote kuanzia Ukraine hadi Myanmar, mpaka Afghanistan, kuanzia Sahel Afrika hadi Yemen wanawake na wasichana ndio wanaolipa gharama kubwa, hivyo kuna haja ya vita na machafuko kukomeshwa mara moja.

Mbali na vita Bi. Bahous amekumbusha kwamba janga la Covid-19 limezidisha pengo la usawa na kuwatumbukiza mamilioni ya wanawake na wasichana katika umasikini mkubwa huku likirejesha nyuma pia hatua zilizopigwa katika sekta za ajira, afya na elimu.

Kwa upande wake Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema katika ujumbe wake kuwa, pamoja na mchango wao mkubwa katika kila nyanja ya maisha fadhila wanazolipwa ni kidogo sana hali ambayo amesema inapaswa kubadilika kuanzia sasa.

Amesema,“kuanzia sasa kwenye siku hii ya kimataifa ya wanawake, ni wakati wa kusongesha mbele mshale wa saa, kwa kila mwanamke na msichana , kupitia hakikisho la elimu bora kwa kila msichana ili waweze kujenga maisha wayatakayo na kuifanya dunia kuwa mahala bora kwetu sote.

342/