Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Hossein Amir-Abdollahian, aliyasema hayo jana Jumatano katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari aliofanya mjini Moscow pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov na akaongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshabainisha wazi misimamo yake kuhusu Ukraine katika ngazi ya juu kabisa.Amir-Abdollahian alisema, katika suala la Ukraine, baadhi ya masuala yanapewa uzito yakiwemo ya kibinadamu, ya mateka wa kivita na mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia na inapasa zitumiwe fursa na uwezo wote uliopo kuondokana na hali iliyopo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa, Iran ambayo ni miongoni mwa wahusika wakuu duniani katika suala la utumiaji nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani iko tayari kutoa msaada na ushirikiano wowote unaohitajika ili kurejesha usalama katika kinu hicho cha nyuklia na maeneo yanayokizunguka.
Aidha Amir-Abdollahian ameashiria mazungumzo ya uondoaji vikwazo na jinsi Iran ilivyo na nia ya dhati ya kufikia makubaliano thabiti na endelevu; na akasisitiza kwamba, ikiwa Marekani itachukua hatua kwa kuzingatia uhalisia wa mambo na kuifanya imara hati iliyopendekezwa, makubaliano hayatakuwa mbali kufikiwa.Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov alisema Moscow imeridhika kikamilifu na hati rasmi ya ufufuaji makubaliano ya nyuklia katika awamu hii ya sasa.Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Russia wametilia mkazo pia suala la kupanuliwa ushirikiano wa nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali.../