Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Sayyid Ebrahim Raisi amesema hayo katika Kongamano la Taifa la Mantiki ya Kuyajenga Upya Mapinduzi na muundo wa kiutamaduni humu nchini na kuongeza kuwa, daima nyoyo safi za vijana na utambulisho wao wa Kiislamu na Kiirani unakumbwa na mashambulizi ya kiutamaduni ya maadui.
Ameongeza kuwa, utambulisho wa kiutamaduni ndilo chimbuko la nguvu za kila taifa na kusisitiza kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu kwa hakika ni mapinduzi ya kiutamaduni, Jamhuri ya Kiislamu nayo kwa hakika yenyewe ina utamaduni wake maalumu na muda wote imekuwa ikiendeleza na kupigania ustawi na maendeleo ya kiutamaduni.
Rais Raisi ameongeza kuwa, katika kimbunga hiki cha vita vya mitandaoni, nchi yenye utamaduni tajiri na imara huwa haitetereki. Hivyo hakuna haja ya kuwa na hofu na ustawi na maendeleo ya elektroniki kwani kila siku huwa kunazuka vitu vipya na inabidi kuwa na wasiwasi pale tu utambulisho wa kitaifa unapokuwa hatarini.
Kabla ya hapo yaani juzi Alkhamisi, Rais Ebrahim Raisi alikosoa uingiliaji wa madola ya Magharibi katika masuala ya ndani ya nchi za Asia Magharibi na kusisitiza kuwa, uingiliaji huo kamwe hauwezi kuwa suluhu ya matatizo na changamoto za eneo hili.
Alisema hayo baada ya kurejea humu nchini kutoka Astana, mji mkuu wa Kazakhstan, alikokwenda kushiriki mkutano wa sita wa wakuu wa nchi wanachama wa "Maingiliano na Hatua za Kujenga Hali ya Kuaminiana Barani Asia" (SICA).
342/