Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Sayyid Ebrahim Raisi alisema hayo leo Ijumaa mkoani Bushehr, kusini mwa Iran na kuongeza kuwa, leo hii taifa la Iran lina uhuru, linajitegemea na lina nguvu zake lenyewe za kijeshi ndani ya mfumo wa demokrasia ya kidini. Wananchi wa Iran wamepata maendeleo katika nyuga tofauti kwa kaulimbiu yao kuu ya "Tunaweza" na wametia nia ya kweli ya kulinda heshima na uhuru wao.
Amezungumzia pia namna taifa la Iran lilivyojihami kishujaa na kuwashangaza maadui katika vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ilikuwa ndiyo kwanza imeundwa wakati huo akisisitiza kuwa, vita mseto vya adui vina lengo la kukwamisha maendeleo ya Iran ya Kiislamu katika nyuga za kiuchumi na kijeshi, lakini vimefeli.
Rais Raisi amezungumzia pia vita vya kipropaganda vya adui vyenye lengo la kueneza chuki dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuzusha hofu na unyonge katika nyoyo za wanafunzi na familia zao humu nchini na amesisitiza kuwa, ametoa amri kwa Waziri wa Usalama wa Taifa na Waziri wa Mambo ya Ndani kufuatilia haraka na kutoa ripoti kamili kuhusu matukio ya hivi karibuni katika skuli za baadhi ya miji humu nchini ambapo hali za kiafya za baadhi ya wanafunzi ziliharibika wakiwa shuleni.
342/