11 Julai 2023 - 19:34
Qalibaf: Changamoto ya sasa ya Magharibi ni kurejea Asia katika kitovu cha nguvu za kiuchumi na kisiasa duniani

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa moja ya changamoto kuu zinazoukabili mfumo wa kimataifa wa mhimili wa Magharibi katika karne ya 21 ni suala la kurejea Asia na kuwa kitovu cha sera za dunia na nguvu za kiuchumi na kisiasa.

Mohammad Baqer Qalibaf Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ameeleza haya leo Jumanne katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Uratibu na Bajeti ya Umoja wa Mabunge ya Asia Tehran.

Mkutano huo umeanza leo hapa Tehran kwa uwenyeji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Wawakilishi wa mabunge ya karibu nchi 20 za Asia wanashiriki katika mkutano huo. 

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kusema kuwa: Njia ya kufikia lengo hili kuu na la kihistoria ni kuanzisha ushirikiano wa kimataifa katika muktadha wa mshikamano wa kikanda.   

Usimamizi wa mzunguko huu wa kihistoria ni uanzishwaji wa ushirikiano wa pande kadhaa katika muktadha wa mshikamano wa kikanda. Qalibaf amesema, nchi za Asia zinaweza kukamilishana na kuwapa watu wa Asia utambulisho wa kipekee katika mfumo wa umoja wenye matabaka tofauti katika karne ya sasa. 

Katika upande mwingine, Spika wa Bunge la Iran  amelaani vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu huko Sweden na kueleza kuwa: Serikali ya Stockholm haiwezi kuhalalisha kivyovyote vile kitendo cha kuvidhalilisha vitabu vitakatifu, matukufu ya dini na Qur'ani Tukufu. Qalibaf ameongeza kuwa, kwa mujibu wa mikataba na makubaliano ya kimataifa kama vile Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu, aina yoyote ya matusi na kudhalilisha dini na mienendo yoyote isiyofaa dhidi ya watu au makundi ya watu wka sababu ya dini yao imetangazwa kuwa hairuhusiwi na kupigwa marufuku; lakini wale wanaodai kutetea haki za binadamu wamekataa hata kulaani tu kwa maneno kitendo kiovu cha kuvunjiwa heshima Qur'ani nchini Sweden kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza.

342/