7 Septemba 2023 - 15:11
 Rais Raisi: Kasi ya mwenendo wa maendeleo ya Iran katika nyuga tofauti inaongezeka

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Iran inaendelea kwa kasi kupiga hatua za maendeleo katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran Press, Seyed Ebrahim Raisi, aliyasema hayo jana Jumatano jioni katika safari yake mkoani Khorasan Kusini (Mashariki ya Iran) katika mkutano na wanazuoni, maimamu wa Ijumaa na wa Sala za jamaa wa mkoa huo, ambapo sambamba na kueleza kwamba katika kipindi cha kuasisiwa, cha uthabiti na maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran maadui wamefanya juu chini kuzuia kufikiwa malengo ya Iran ya Kiislamu, amebainisha kuwa: baada ya maadui kujionea wenyewe kwamba licha ya vizuizi, uafriti na uzushaji fitna Jamhuri ya Kiislamu imekuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengine na imegeuza vikwazo na mashinikizo kuwa fursa na kupiga hatua katika nyanja mbalimbali, waliamua kuzusha fujo na machafuko.  

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, vita vya leo ni vita vya irada; na adui anataka kututwisha irada na matakwa yake kupitia vyombo vya habari, lakini kama ambavyo taifa la Iran limeweza hadi sasa kuibuka mshindi dhidi ya njama kadha wa kadha za adui, bila shaka yoyote litaibuka tena mshindi katika medani hii.

  Seyed Ebrahim Raisi, aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Shahid Kaveh mjini Birjand jana asubuhi na kulakiwa na mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu mkoani Khorasan Kusini, Gavana, wabunge kutoka mkoa huo na maafisa wengine wa mkoa.../

342/