2 Oktoba 2023 - 19:17
Kutoka muqawama wa silaha katika Ukingo wa Magharibi hadi kuanza tena kwa maandamano ya haki ya kurejea wakimbizi huko Gaza

Katika muendelezo wa vitendo vya walowezi wa Kizayuni vya kuuvunjia heshima Msikiti wa Al-Aqswa katika siku chache zilizopita kwa kisingizio cha sikukuu za Kiyahudi, Jumapili asubuhi ya jana, watu hao walifanya vitendo vya uchochezi katika eneo hili takatifu baada ya kuingia humo kinyume cha sheria. Walowezi wa Kizayuni wa mrengo wa kulia walianza kucheza, kurukaruka huku wakiimba kwenye lango la Msikiti wa Al-Aqsa.

Hapo awali, makundi ya walowezi yenye misimamo mikali yalitoa wito wa hujuma na mashambulizi makubwa dhidi ya Msikiti wa Al-Aqswa wakati wa sikukuu za pande tatu ambazo zilianza Septemba 17 na ambazo zitaendelea hadi katikati ya mwezi huu wa Oktoba. Hatua hizi za kichochezi zilikabiliwa na radiamali ya makundi ya muqawama ya Wapalestina kuanzia Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hadi katika Ukanda wa Gaza.

Katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, makundi ya muqawama yalifanya operesheni 14 dhidi ya Wazayuni katika maeneo tofauti ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan katika muda wa saa 24 zilizopita. Operesheni za vikosi vya muqawama zilifanyika Quds, Nablus, Tulkarm, Qalandia, Jenin, Qalqilya, Ramallah na al-Khalil.

Katika Ukanda wa Gaza, vijana wenye kusimama kidete wa ukanda huo walionya kwamba, Msikiti wa Al-Aqswa ukiwa sehemyu ambayo Mtume aliondokea kwenda katika safari ya Miraj ni mstari mwekundu na iwapo wavamizi watauvamia msikiti huo mtakatifu na Wapalestina walioko ndani yake, moto wa muqawama katika mipaka ya Gaza utawaka tena. Kinachoongeza umuhimu wa onyo hili ni kuanza tena kwa maandamano ya "haki ya kurudi" hadi Gaza baada ya 2020.Katika miaka ya 2018 hadi 2020, maandamano ya mtawalia ya kurudi katika Ukanda wa Gaza yaligeuka na kuwa jinamizi kwa utawala huu, haswa walowezi wa Kizayuni walioko kando kando yake. Mnamo Machi 30, 2018, sambamba na "Siku ya Ardhi" (Yaum al-Ardh) huko Palestina, idadi kubwa ya Wapalestina waliokuwa wakiishi kambi za Wapalestina walihama kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya Palestina kuelekea kwenye mipaka ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Kauli mbiu ya Wapalestina hao ilikuwa ni ombi la kurejea katika nchi yao. Kutokana na kuwa mbali kambi za Wapalestina kutoka mipakani, maandamano ya kurudi baada ya "Siku ya Ardhi" ya 2018, yalifanyika tu katika Ukanda wa Gaza, kwa lengo la kuvunja mzingiro dhidi ya eneo hilo na yaliendelea hivyo kila wiki mpaka mwishoni mwa mwaka 2020.

Kuanzia Machi 2018 hadi mwisho wa 2020, Wapalestina 215 waliuawa shahidi na jeshi la utawala haramu wa Israeli kwenye mipaka ya Ukanda wa Gaza na maeneo yanayokaliwa kwa mabavu mnamo 1948, na takriban 50 kati yao walikuwa watoto. Pia, watu wapatao 20,000 walijeruhiwa katika maandamano hayo, na takriban 5,000 kati yao walikuwa watoto.

Ijapokuwa hali ya Gaza imepungua kwa kiasi fulani baada ya wiki mbili za maandamano ya "Haki ya Kurejea" kufuatia upatanishi wa Qatar na kusalimu kwa utawala wa Kizayuni kuhusu kukifungua tena kivuko cha Iriz, lakini kuendelea kwa vitendo vya kichochezi vya Wazayuni huko katika msikiti wa al-Aqswa kunaweza kupelekea kushadidi pia hali ya mambo.Kwa mujibu wa Kanali ya 13 ya utawala huo ghasibu, mamlaka za Israel zililazimika kufunga vivuko vya Gaza kufuatia maandamano ya haki ya kurejea katika mipaka ya mashariki ya Ukanda wa Gaza na kurushiana risasi ndani ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, lakini hatimaye wakasalimu amri kwa Hamas na kufungua vivuko ili wafanyakazi wa Kipalestina waingie katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wasiwasi mkubwa wa Wazayuni kuhusu maandamano ya haki ya kurejea ni kupanuka kwa wigo wa maandamano haya katika maeneo mengine. Wasiwasi mkubwa wa Wazayuni ni kwamba, Wapalestina wengine hususan Wapalestina wanaoishi katika kambi nje ya Palestina wataona kwamba "Maandamano ya Haki Kurejea" yamekuwa na natija na wanaweza kurejea Palestina kwa kutumia silaha hii. Pamoja na hayo, iwapo chokochoko za Wazayuni waliochupa mipaka zitaendelea katika Msikiti wa Al-Aqsa, kwa kuzingatia onyo la makundi ya muqawama, kutakuwa na uwezekano wa kuanza tena maandamano ya haki ya kurejea na hivyo kuibuka mizozo na mapigano katika Ukanda wa Gaza.

342/