15 Oktoba 2023 - 20:30
Ebrahim Raisi: Kimbunga cha al-Aqswa ni upanga uliotolewa katika ala yake baada ya kushadidi jinai za Wazayuni

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Kimbunga cha al-Aqswa ni upanga uliotolewa katika ala yake baada ya kushadidi jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Rais wa Iran amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Sultani wa Oman Haitham bin Tariq ambapo sambamba na kusisitiza kwamba, Tehran daima imekuwa ikizingatia na kulipa umuhimu suala la kupanua mashirikiano, kuimarisha ujirani mwema na kuinua kiwango cha kuaminiana baina ya nchi mbili amesifu nafasi ya Oman katika kutatuliwa mizozo ya kieneo na kimataifa.

Ebrahim Raisi ameongeza kuwa, hii leo utawala wa Kizayuni na waitifaki wake kwa kuendelea kukata maji na umeme na kuzuia kuingia kwa dawa na chakula wanafuatilia mauaji makubwa huko Gaza na kuwalazimisha watu kuondoka majumbani mwao kwa umati.

Sambamba na kuashiria kuwa, uungaji mkono usio na kikomo wa nchi za Magharibi na hasa Marekani kwa jinai za Wazayuni kumeifanya hali kuwa ngumu na ya kutisha zaidi, Ebrahim Raisi ameitaja hatua madhubuti na ya haraka ya nchi za Kiislamu na watu huru wa dunia kuwa ni muhimu kwa ajili ya kusimamisha mashine ya mauaji ya Wazayuni.Katika mazungumzo hayo ya simu, Sultani wa Oman sanjari na kushukuru misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuwatetea wananchi madhulumu wa Palestina amesema: Tusiruhusu kutokea kwa mara nyingine tena siasa za kuwafukuza watu wanaodhulumiwa wa Palestina na kuwalazimisha kuyahama makaazi yao. Sultani wa Oman ameunga mkono mtazamo wa Rais wa Iran kuhusu nguvu nauwezo wa Umma wa Kiislamu wa kukomesha dhulma na ukatili unaoendelea huko Gaza, na akasema: Tunawasiliana na pande zote zinazoweza kuwa na mchango na nafasi muhimu katika kusitisha jinai hizi.