23 Oktoba 2023 - 15:59
Watu waliozingirwa Gaza wanasubiri msaada wa kimataifa

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema katika hotuba yake kwenye Kikao cha Amani cha Cairo: 'Tunakutana katikati ya eneo ambalo lina maumivu makali na limesimama hatua moja kutoka kwenye shimo refu. Eneo ambalo hauwezi kukosa kuhuzunika na kukereka na moyo kuuma na kusononeka kwa kuona picha za machungu na mateso ya watu wake.'

Waziri Mkuu wa Iraq Mohammad Al-Sudani amesema katika kikao hicho hicho cha Cairo: "Lau maneno ya taifa lenye haki halali yangesikilizwa na maazimio ya kimataifa kuheshimiwa, suala la Palestina lisingefikia hatua hii. Iraq inapinga suala la kuhamishwa kwa lazima Wapalestina kutoka Ukanda wa Ghaza na wakazi wake kuondoshwa makwao.Tunataka  usitishwaji vita na kufunguliwa kwa vivuko ili misaada iwafikie haraka wakazi wa Ghaza na kisha kubadilishana mateka na wafungwa."

Tangu kuanza kwa operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa siku 16 zilizopita sawa na Oktoba 7, kushambuliwa maeneo ya makazi na umma kwa upande mmoja na kukatwa maji, umeme na uhaba mkubwa wa chakula na dawa kwa upande mwingine, kumewafanya wakazi wa Ukanda wa Ghaza kukabiliwa na hali ngumu sana na kupelekea taasisi za haki za binadamu kutangaza hali ya kibinadamu katika eneo hilo kuwa mbaya na ya kutisha. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiwemo Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, Mfuko wa Idadi ya Watu wa Umoja wa Mataifa, UNICEF, Mpango wa Chakula Duniani na Shirika la Afya Duniani yamesema katika taarifa ya pamoja kwamba: "Tunatoa wito wa kusitishwa mapigano, pamoja na kufikishwa haraka misaada ya kibinadamu huko Ghaza, ili wanaoshughulikia misaada ya kibinadamu waweze kutoa huduma kwa  wananchi wanaohitaji msaada, kuokoa maisha na kuwazuia kuendelea kupata mateso zaidi."