21 Desemba 2023 - 15:10
Dalili za usitishaji mpya wa mapigano huko Gaza katika siku ya 75 ya Kimbunga cha Al-Aqsa

Katika siku ya 75 ya operesheni ya kimbunga cha al-Aqsa, utawala wa Kizayuni umeanzisha tena mashambulizi makali ya anga katika maeneo ya mashariki na kusini mashariki mwa Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Utawala wa Kizayuni umeshambulia nyumba ya familia ya Hamdan katika kambi ya wakimbizi huko Khan Yunis iliyoko kusini mwa Gaza, na kuwaua shadidi Wapalestina 14.

Katika hali ambayo utawala ghasibu unashambulia kwa mabomu maeneo ya makazi na vituo vya matibabu katika Ukanda wa Gaza, msemaji wa shirika la UNICEF linalofungamana na Umoja wa Mataifa amesema kuwa vita hivyo ni vita vya kuwaua kikatili watoto.

James Alder amesema: Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, idadi ya wahanga imefikia watu 19,000, ambapo asilimia 40 jati yao ni watoto. Idadi kubwa ya watoto wanaouawa katika vita ndiyo imepelekea UNICEF kuviita vita hivyo kuwa ni vita vilivyo dhidi ya watoto, na iwapo vitaendelea kwa siku au wiki nyingine kadhaa zijazo, tutashuhudia watoto zaidi wakipoteza maisha kutokana na uzembe (unaofanywa na jami ya kimataifa) au magonjwa. Usitishwaji mapigano ndio njia pekee ya kuzuia watu kufa kwa magonjwa au njaa.Kushadidi hali ya kibinadamu huko Gaza, kwa upande mmoja, na kushindwa jeshi la Kizayuni kufikia malengo yake ya kijeshi katika vita vya nchi kavu na kupata hasara katika vita kumepelekea utawala huo kujadili uwezekano wa usitishaji vita mpya na kuanza tena mashauriano katika uwanja huo.

Kuhusiana na hilo, baadhi ya vyanzo vya habari vimeashiria safari iliyofanywa jana Jumatano na Ismail Haniyeh, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, mjini Cairo.

Vyombo vya habari vya Kiibrania vimetangaza habari zinazogongana kuhusu mazungumzo hayo, ambapo kwa mujibu wa gazeti la Ha'aretz, mjumbe huyo wa Hamas ameelekea Cairo kwa mara ya kwanza baada ya kuanza vita. Cairo na Doha hata hivyo zinasema kuwa suala la kubadilishana mateka haliwezi kutatuliwa katika muda mfupi.

Gazeti la Aharanot kwa upande wa pili limeripoti kwamba Israel kwa sasa inajaribu kutekeleza misingi mitatu katika mazungumzo hayo, yaani kufanya mazungumzo ya usitishaji vita na wakati huo huo kuendeleza vita, kuendeleza mazungumzo kutokea pale yaliposimamia katika duru ya kwanza na tatu ni kuainishwa makundi maalumu ya mateka watakaoachiliwa huru.

Kama ilivyoripotiwa na shirika la habari la Sputnik, Rais wa Israel Isaac Herzog alisema Jumanne kwamba Israel iko tayari kwa usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza ili kuachiliwa huru mateka waliosalia.

Tovuti ya Walla ikiwanukuu maafisa wa Israel na duru ya kigeni imeripoti kuwa, utawala wa Kizayuni umemuarifu mpatanishi wa Qatar kuhusu utayari wake wa kusimamisha vita kwa muda wa wiki moja.

Viongozi wa Hamas wamesisitiza mara kadhaa kwamba hawatajadili makubaliano ya kubadilishana mateka kabla ya usitishaji vita wa kudumu na kusimamishwa kabisa vita.

Kwa upande mwingine, mashauriano ya kuweka usitishaji vita na kuzuia Marekani kutumia  kura ya turufu kupinga usitishaji vita huo yameanza tena katika Baraza la Usalama.

Desemba 17 mwezi huu, Marekani ikiwa ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ilipinga azimio lililopendekezwa na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambalo lilitokana na ombi la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, la kutaka kusitishwa mapigano katika Ukanda wa Gaza, licha ya kupata uungaji mkono mkubwa wa kura 13 katika baraza hilo.Kati ya kura 15 za wajumbe wa Baraza la Usalama, azimio lililopendekezwa na UAE lilipata kura 13 za ndio, moja ya hapana kutoka kwa Marekani na nyingine ya Uingereza ambayo ilijizuia kupiga kura, ambapo hatimaye lilipingwa na Washington kupitia kura ya turufu. Hatua hiyo ya serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani ililalamikiwa vikali kimataifa. Hatua hiyo ya ubabe wa Marekani na utawala haramu wa Israel imeyapelekea makundi ya muqawama katika eneo kuchukua hatua dhidi ya pande hizo zinazotumia mabavu dhidi ya mataifa mengine, na hivyo kupanua wigo wa vita na kuvifanya vichukue mwelekeo wa kieneo. Wakati huo huo uchumi wa utawala wa kibaguzi wa Israel unakabiliwa na hatari kubwa ya kusambaratika kutokana na kuhatarishwa usalama wa meli zake za kibiashara katika maji ya Bahari ya Sham.

342/