Umahd (Al-Mahdawiyya) ni asili ya Kiislamu ambayo Madhehebu zote "Shia na Sunni" wanaikubali; kwa sababu kuanzia kwa Mtume Kipenzi wa Uislamu (Rehema na Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake) hadi kwa Imam wa 11, Imam Hasan al_Askari (Amani iwe juu yake), utapata kuna hadithi nyingi mno zinazoelezea kuhusu sifa na fadhila za Imam Mahdi (a.t.f.s).
Chanzo bora cha kujua sifa na pointi za msingi (za kiupendeleo) za "Mahdism" (Umahdi) ni Hadithi hizi.
Miongoni mwa Maasumina (a.s), Hadithi za Mtukufu Baba wa Imam wa Zama kuhusu Mwanawe zina nafasi muhimu sana.
Katika kuelezea sifa za Hadhrat Mahdi (a.t.f.s), tutasimulia / tutabainisha Hadithi kutoka katika Hadithi za Imam Hasan al_Askari (a.s):
Ahmad bin Is'haq amesema:
Nilimsikia Abu Muhammad Hasan bin Ali al-Askari (a.s) akisema:
"الحمد للّه الذي لم يخرجني من الدنيا حتى أراني الخلف من بعدي، أشبه الناس برسول الله صلى اللّه عليه وآله خَلقاً وخُلقاً، ويحفظه اللّه تبارك وتعالى في غيبته، ثم يظهره فيملأ الأرض عدلاً وقسطاً كما مُلئت جوراً وظلماً"
"Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu ambaye hakunitoa hapa Duniani mpaka nimwone (anionyesha) mrithi wangu, Mwenye kufanana zaidi na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kuliko watu wote, katika uumbaji (maumbile) na maadili. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amhifadhi katika Ghaiba yake, na kisha amdhihirishe, ili aje kuijaza ardhi Haki na Uadilifu, kama ilivyojaa dhulma na udhalimu".
Ghaiba na Kudhihiri
Kwa mujibu wa hotuba hii ya Imamu wa 11 (a.s), Imamu wa 12 (a.t.f.s) atakuwa na 'Ghaiba na Kudhihiri'.
Katika sentensi yake aliposema:
"يحفظه اللّه تبترك وتعالى في غيبته، ثم يظهره"
"Mwenyezi Mungu atamlinda na kumhifadhi Imam Mahdi (a.t.f.s) katika Ghaiba yake na kisha atamdhihirisha tena".
Kuna nukta tatu katika sentensi hiyo:
1_ Mwenyezi Mungu kumhifadhi Imam wa Zama".
2_Ghaiba ya Imam.
3_Kudhihiri kwa Imam.
Kwamba Mwenyezi Mungu atamlinda na kumhifadhi Imam katika zama za Ghaiba yake, na kisha kumfanya aonekane / adhihiri machoni kwa watu na awe baina ya watu Katika dhahiri.
Zama / Wakati wa Ghaiba na kuonekana / kudhihiri tena kwa Imam wa Zama, hilo lipo mbele ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Ta'ala.
Mwenyezi Mungu atamuweka katika Ghaiba (Hali ya kutokuonekana katika macho ya watu) na kumuhifadhi, na Imam wa zama atakuwa na umri mrefu, na kisha Mwenyezi Mungu atamdhihirisha (baina ya watu, na wataweza kuishi naye na kumuona katika dhahiri), kwa hivyo hakuna mtu (yeyote yule) anayejua kiwango cha wakati wa Ghaibu na wakati wa kuonekana (kudhihiri) tena kwa Imam wa Zama ispokuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t); na si sahihi kubainisha muda / wakati wa kutokea (kudhihiri) kwa Imam wa Zama.
Kuanzisha Haki ya Ulimwengu.
Kupitia Mapinduzi Makubwa zaidi ya Ulimwengu, Imam Mahdi (a.t.f.s) ataanzisha Serikali ya Kiislamu itakayoenea zaidi Ulimwenguni, na kuanzisha / kuasisi Haki na uadilifu Ulimwenguni.
Wakati ambao Ulimwengu utakuwa umegubikwa na dhuluma na udhalimu, Qaim Aali Muhammad (a.t.f.s) atadhihiri ili Haki na Usawa viweze kutawala Ulimwenguni.
Dhulma na Ukandamizaji wa Kiulimwengu sio mfumo endelevu wa kudumu na kuutawala Ulimwengu, na Haki na Uadilifu wa Ulimwengu wa Umahdi utachukua nafasi yake (kwa maana: Utachukua nafasi ya dhulma na Ukandamizaji huo).
Katika kauli yake aliposema:
(فيملأ الأرض عدلاً و قسطاً كما ملئت جوراً و ظلماً).
Tunaupata ukweli / uhakika huo uliotajwa hapo juu katika sentensi hiyo kwamba: "Atakuja kuijaza Dunia / Ulimwengu Haki na Uadilifu, kama ulivyojaa Dhulma, udhalimu na Ukandamizaji".
Masahaba wa Imam Mahdi (a.t.f.s) na wale wanaosubiri / wanaongejea kudhihiri kwake, wote kwa ujumla wanangojea uadilifu wa ulimwengu wa Mahdawiyyah (au) Umahdi, na inafaa daima kutafuta Haki na kuchukua hatua madhubuti kuelekea kusimamisha Haki na Uadilifu.
Katika historia ya maisha ya Mwanadamu, "Dhulma na Uadilifu" vimekuwepo daima katika Historia ya Mwanadamu katika pande mbili za, Haki na Batili.
Watu wanaosimama upande wa Uadilifu wa Umahdi, kamwe hao hawatendi dhulma na ufisadi, na wanasonga mbele kuelekea kwenye ukamilifu bora wa Kiulimwengu wa Umahdi na uadilifu wa Ulimwengu mzima.
Ni wajibu kwa kila mtu kupigana na dhulma na Ukandamizaji kwa kadiri ya uwezo wake; na kwa hakika dhulma hairuhusiwi kwa wakati wowote ule.
................................................
_ Kefayyat al-Athar fi Nassi Alal - Aimmat al-ithnay Ashar: Karne ya 4, Ukurasa wa 295.
- Kamal al-Din wa Tamam al-Niimat: Sheikh Sadouq. Juzuu ya 2, Ukurasa wa 409.
- Al-Sirat al-Mustaqim ila Mustahiqqi al_Taqdeem, karne ya 9, Ukurasa wa 144.
- Bihar al-An'war: Juzuu ya 54, Ukurasa 161.
Makala ya Hojjat al-Islam Javaheri, Mwanachama wa Kitivo cha Chuo Kikuu cha Ferdowsi (Iran).